Wasimamizi MV. Nyerere wahojiwa


SERIKALI inawashikilia na kuwahoji maofisa wote waliokuwa wanakisimamia kivuko cha MV. Nyerere kilichosababisha vifo vya watu 224.

Kivuko hicho kilizama umbali wa mita 50 kabla ya kutia nanga katika gati la bandari ndogo ya Ukara, Alhamisi wiki iliyopita majira ya saa 8:05 mchana ikitokea Bugorora kuelekea Kisiwa cha Ukara, wilayani Ukerewe.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, aliyasema hayo jana katika viwanja vya Shule ya Sekondari Bwisya, wakati akiongoza mamia ya wananchi kwenye mazishi ya watu tisa waliofariki katika ajali hiyo.

Akizungumza kwenye mazishi hayo, Majaliwa alisema maofisa wote waliokuwa wanahusika kukihudumia na kukisimamia kivuko hicho wameshakamatwa na vyombo vya dola na wanahojiwa.

"Maofisa wote pamoja na wanaohusika na usafiri wa majini kwenye kivuko hicho tumeshawakamata na taratibu za mahojiano zinaendelea," alisema Majaliwa.

Majaliwa alisema mbali na kukamatwa kwa watu hao, serikali itaunda tume ya kuchunguza tukio zima la ajali hiyo, ili kuwabaini watu waliohusika na uzembe wa kutokea kwa ajali hiyo ili nao washughulikiwe.

Alisema timu ya tume hiyo itatangazwa muda wowote na itakapokamilika itaanza kazi mara moja ya kubaini tukio zima la ajali.

Aidha, Majaliwa alisema kwa sasa serikali iko katika utaratibu wa kutafuta kivuko kingine mbadala kitakachotumika kuwasafirisha wakazi wa Ukerewe wakati kivuko cha MV. Nyerere kilichozama kikiwa katika taratibu za kuondolewa kwenye maji.

Katika kuwafariji wafiwa, Majaliwa alisema serikali itatoa Sh. 500,000 kwa kila mfiwa ili kusaidia kusafirisha miili pamoja na kuratibu shughuli zote za mazishi.

"Kwa sasa zoezi la uokoaji linaendelea, meli itavutwa hadi ufukweni na tutaendelea na mazishi, nitaendelea kubaki hapa ili kuendelea kusimamia na kuhakikisha linakwenda vizuri," alisema Majaliwa.

Majaliwa alisema hadi jana mchana waokoaji waliokoa watu 41, na kati ya miili 224 ya waliofariki,  219 imetambuliwa na ndugu, 214 ilichukuliwa.