Wauguzi watakiwa kuchunga lugha wanapohudumia wagonjwa


Wauguzi na wakunga wametakiwa kuwa na lugha nzuri kwa wagonjwa wanapowahudumia kwani kauli hizo ni sehemu muhimu ya tiba.

Hayo yalielezwa na Mkuu wa Chuo cha Uuguzi na Ukunga cha Massana, Hamis O. Mwenda, katika mahafali ya 12 ya stashahada na tisa ya cheti katika chuo hicho yaliyofanyika wiki hii jijini Dar es Salaam.

Katika mahafahali hayo ambayo wahitimu 82 walikabidhiwa vyeti wakiwamo 25 wa stashahada na 57 wa cheti, pia walitakiwa kuwa kioo cha jamii kwa tabia nzuri kazini na katika jamii, kufanya kazi kwa weledi na kufuata maadili ya fani ya uuguzi na ukunga

Mwenda aliwataka wahitimu hao kujiepusha na vitendo vya rushwa watoapo huduma kwa wagonjwa na kuwa na mitazamo chanya kwa wagonjwa wakati wote.

Mkurugenzi huyo alisema kuwa, kwa kutambua mchango wa vyuo binafsi katika sekta ya afya ambao ni kusaidiana na serikali kuboresha huduma za afya nchini, ameiomba serikali itoe ruzuku kwa taasisi binafsi zinazoendesha mafunzo ya afya ili wanafunzi wanaosoma katika vyuo hivyo wapate nafuu ya ada.

Kadhalika, aliomba waalimu waingizwe kwenye mpango wa kuazimwa (Secondment) toka wizarani kama ilivyo kwenye vyuo vya Taasisi za dini na wanafunzi wapewe fursa za ufadhili au mikopo.

Nao wahimimu wa mafunzo hayo katika risala yao iliyosomwa na Neema Mhando na Steven Luwongo walisema kukosekana kwa mikopo kwa wanafunzi wa uuguzi na ukunga kumekuwa ni changamoto kubwa kiasi cha kuwafanya wengine kukatiza masomo. Waliomba serikali iwasaidie mikopo ya elimu.

Kadhalika, waliomba serikali kuwapangia vituo vya kazi kwani kuchelewa sana kupatia fursa hizo husababisha baadhi yao kujiajiri katika kazi zilizo nje ya fani zao, licha ya uhitaji mkubwa wa uuguzi na ukunga katika jamii.