Yanga wapewa mbinu ya kuwadhoofisha Simba


Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili na Mashindano katika klabu ya Yanga, Hussein Nyika, amesema kikosi chao kipo tayari kwa mchezo wa leo dhidi ya Singida United.

Yanga itakuwa ina kibarua kizito mbele ya Singida majira ya saa 1 jioni ikiwa imetoka kujeruhiwa na African Lyon kwa kufungwa mabao 3-2.

Nyika amesema wao wanatambua kuwa Singida ilitoka kufungwa na Lyon lakini watapigana kulingana na namba Kocha Mkuu, Mwinyi Zahera alivyowaandaa wachezaji wake.

Aidha, Nyika amewataka mashabiki wa Yanga kujitokeza kwa wingi katika mchezo dhidi ya watani zao wa jadi Simba utakaopigwa Septemba 30 2018.

Nyika ameeleza ujio wa mashabiki na wanachama wengi kwa wingi uwanjani utachangia kuwadhoofisha Simba kwa sababu hamasa itakuwa kubwa ndani ya Uwanja.

"Ni vema mashabiki na wanachama wetu wakaja kwa wingi zaidi kwenye mechi yetu na Simba, leo tunamalizana na Singida kisha tutajiandaa kukabiliana na Simba Septemba 30" alisema.