https://monetag.com/?ref_id=TTIb Akamatwa na Polisi akisafirisha dawa za kulevya kwenye msafara wa msiba | Muungwana BLOG

Akamatwa na Polisi akisafirisha dawa za kulevya kwenye msafara wa msiba


Na Rashid Nchimbi wa Polisi Arusha
Jeshi la Polisi mkoani hapa limemkamata kijana mmoja jina linahifadhiwa mkazi wa Daraja Mbili halmashauri ya jiji la Arusha akiwa na kilogramu 207 za madawa ya kulevya aina ya Mirungi.

Akitoa taarifa hiyo mapema leo ofisini kwake, Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Ramadhani Ng’anzi alisema kwamba, mtuhumiwa huyo alikamatwa jana saa 6:00 Mchana akiwa anatokea mpakani mwa mkoa wa Kilimanjaro kuingia mkoa wa Arusha ambapo alitumia mbinu mpya ya usafirishaji wa madawa hayo kwa kujipachika katikati ya msafara wa magari yaliyokuwa yanakwenda msibani.

Kamanda Ng’anzi alisema kwamba Jeshi hilo lilipata taarifa juu ya uwepo wa mtu huyo aliyekuwa anasafirisha Mirungi kwa kutumia gari ndipo walipowapeleka askari haraka katika eneo la Kikatiti wilayani Arumeru na kuweka mtego.

“ Wakiwa katika eneo hilo baada ya muda askari hao waliona gari aina ya Suzuki Escudo rangi ya Kijivu lenye namba za usajili T 505 CNC likiwa katikati ya msafara wa magari yaliyokuwa yanaelekea msibani lakini kwa umahiri mkubwa walilibaini ndipo wakalizuia”. Alifafanua Kamanda Ng’anzi.

Kamanda Ng’anzi alisema kwamba baada ya kufanya upekuzi waligundua kuwepo kwa madawa hayo yaliyohifadhiwa nyuma ya “boot” yakiwa yamehifadhiwa kwenye viroba tofauti tofauti vyote vikiwa na uzito wa kilogramu 207.

Katika hatua nyingine jeshi hilo limewakamata watu 12 ambao walikuwa wanatumia pikipiki kufanya uporaji wa pochi kwa wanawake hasa nyakati za jioni pindi wanapokuwa barabarani.

Kamanda Ng’anzi alisema kwamba watuhumiwa hao wamekamatwa kufuatia operesheni kabambe inayoendeshwa na Jeshi hilo mkoani hapa hasa kuelekea mwishoni mwa mwaka.

Akitaja pikipiki hizo zilizopatikana kutokana na msako huo ni MC 468 BDK, MC 807 APW, MC 436 BFU, MC 621 BJM zote aina ya Toyo huku nyingine ni MC 453 BEK aina ya Boxer pamoja na MC 560 BJJ aina ya Fekon.

Alisema mbali na pikipiki hizo pia jeshi hilo lilipata gari aina ya Toyota Noah lenye namba za usajili T 775 DJL ambalo lilitumika kubebea mali zilizoibiwa katika eneo la Njiro.