Chadema yatumia masaa 14 kuwajadili Kubenea na Komu


Haikua kazi rahisi! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA kutumia masaa 14 kwenye kikao chake cha kamati kuu kufanya uamuzi wa kutoa adhabu kwa wabunge wake wawili Saed Kubenea wa Ubungo na Anthony Komu wa Moshi Vijijini.

Wabunge hao walipatikana na hatia ya kutaka kukihujumu chama hicho ikiwemo kupanga mikakati ya kumdhuru Meya wa Ubungo, Boniface Jacob na kutaka kuchunguzwa kwa Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU ambapo wawili hao walikiri makosa hayo yote.

Akizungumza na wandishi wa habari makao makuu ya chama hicho mapema leo, Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho Zanzibar, Salum Mwalimu amesema kuwa kamati kuu ilitumia muda huo wa masaa 14 kuhakikisha kuwa wanatenda haki katika kufanya maamuzi ambayo hayatamuumiza mtu yoyote.

" Tuliwahoji kama ulivyo utaratibu wetu wa kawaida wa kuwauliza na kuwasikiliza na ndio maana mnaona kuwa hakuna yeyote ambaye ametoka mbele yenu na kusema kwamba maamuzi ya kamati kuu hayakuwatendea haki," amesema Mwalimu.

Akizungumzia suala la nafasi ya Mwenyekiti wa Chama hicho, Mwalimu amesema kuwa wao bado wana imani na Mbowe na kwamba kiongozi huyo wa juu ataendelea kuiongoza Chadema hadi pale watakapoona kwamba inatosha.

" Mbowe hajiteui wala hajichagui katika nafasi yake ya Uenyekiti, amekua akichukua fomu na wagombea wengine na kugombea nao kama Katiba ya chama chetu inavyotaka, hajawahi kujiweka katika nafasi hiyo kimabavu, na niwaambie ukweli yeye mwenyewe hataki uongozi ila sisi tunamwambia hapana utatuongoza," amesema Mwalimu.