Jambo hili ni muhimu sana katika safari yako ya mafanikio


Benson Chonya
Kila wakati, pambana na mambo magumu, wakati mambo hayo bado ni rahisi. Pambana na changamoto zako, wakati changamoto hizo bado ni kidogo. Pambana na kuitunza afya yako, wakati bado umzima. Pambana na umaskini, wakati bado ukijana mwenye nguvu.

Kila changamoto unayokutana nayo kwenye maisha, unaweza kuishinda ikiwa utakabiliana nayo mapema. Acha kusubiri mambo yameharibika ndio uanze kukomaa na changamoto yako. Acha kusubiri nyumba imeungua ndio utafute maji ya kuzimia moto.

Jifunze kutokuishi maisha ya zima moto. Ishi kwa mipango sahihi, ambayo mipango hiyo mwisho wa siku itakuongoza wewe kuweza kufikia katika mafanikio yako makubwa. Wengi wanashindwa katika maisha kwa sababu ya kuchelewa kuthibiti mambo ambayo walitakiwa wayathibiti mwanzoni.

Jiulize ni mara ngapi umekwama, kwa sababu ya kushindwa kuithibiti hali fulani ambayo ulitakiwa kuithibiti mapema? Acha kuendelea kuharibu maisha yako kwa kusubiri eti mpaka mambo yameharibika ndio utafute dawa yake. Changamka sasa na anza kutekeleza majukumu yako mapema.