Mbelgiji awashangaa Alliance baada ya ushindi wa 5-1

Kocha, Patrick Aussems

Kufuatia Simba kushusha kichapo cha mabao 5-1 kwa Alliance FC usiku wa jana katika ligi kuu Tanzania bara, kocha mkuu wa mabingwa hao watetezi, Patrick Aussems ameshangazwa na kiwango cha Alliance.

Akizungumza na wanahabari baada ya kumalizika kwa mchezo huo, kocha Patrick Aussems amesema kuwa licha ya pongezi zote wanazopewa Simba lakini wapinzani wao wanahitaji pongezi zaidi kwa namna ambavyo wamecheza.

"Ninashangazwa kuwaona Alliance katika nafasi ya mwisho ya msimamo wa ligi kwasababu wamecheza mpira wa kuvutia, tumekutana na timu nyingi sana zinazocheza mpira, kwahiyo na wao nawapongeza kwa hilo", amesema.

Pia kocha huyo amezungumzia kiwango cha mshambuliaji, Adam Salamba ambaye alianza katika kikosi na kufunga bao lake la kwanza, amesema, "Kwangu mimi sina wachezaji 11 pekee, bali nina kundi la wachezaji 18 kwahiyo kumweka benchi Kagere na kumuanzisha Salamba na kufunga bao ni furaha kwangu", ameongeza.

Baada ya matokeo hayo, sasa Simba inafikisha alama 20 katika msimamo wa ligi kuu ikiwa katika nafasi ya pili mbele ya Yanga iliyo katika nafasi ya tatu na alama 19, huku ikitarajia kushuka dimbani hii leo kucheza na KMC.