Mbunge wa upinzani anayetajwa kwenda CCM afunguka mbele ya Wananchi


Kufuatia kuwepo kwa wimbi kubwa la wabunge na madiwani wa upinzani kuhamia Chama cha Mapinduzi CCM huku yeye mwenyewe akihusishwa kujiunga nacho, Mbunge wa Mtwara Mjini (CUF), Maftaha Nachuma amejitokeza mbele ya wapiga kura wake na kukana tuhuma hizo.

Maftaha amesema yeye maisha yake yote hajawahi kuwa mwanachama wa chama chochote tofauti na CUF hivyo kitendo cha wapinzani wake kisiasa kumuhusisha na kukimbilia CCM ni sawa na kujitekenye na kucheka wenyewe kwani yeye anafahamu nguvu kubwa aliyonayo imetokana na wananchi wake kumuamini.

" Sina sababu yoyote ya kuhama, nyie mliniamini nikiwa CUF sasa nihamie CCM kutafuta nini, ni jambo la aibu niliwaomba kura mwaka 2015 kupitia chama cha wananchi halafu leo niache ubunge nihamie CCM kisha nirudi tena kwenu kuwaomba mnipe ubunge ambao mlinipa hapo awali, ndugu zangu niwaahidi kwamba siwezi kuwa miongoni mwa wanaokimbia vyama vyao," amesema Maftaha.