Mkurugenzi Ilemela atangaza kukamata na kuuza mifugo inayozagaa mjini


Na James Timber, Mwanza

Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela jijini Mwanza imetangaza kukamata na kuuza kwa mnada mifugo kama vile Ng'ombe, Punda, Mbuzi, Kondoo na mingine jamii hiyo endapo itakutwa imezagaa ovyo maeneo ya mjini.

Katika taarifa yake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani hapa, John Wanga imeeleza kuwa kwa mujibu wa ufuguji wa mifugo hiyo itaendana na kibari kutoka halmashauri ambapo anayefuga mifugo aina hiyo anaamriwa kuiondoa mpaka kufikia Oktoba 31, 2018,  atakayekiuka atawajibishwa kisheria bila taarifa zaidi.

Wanga ametahadharisha endapo itatokea mtu au taasisi yoyote itaachia mifugo aina ya Ng'ombe, Mbuzi, Kondo, Punda na mingine inayofanana na hiyo kuzagaa ovyo katika maeneo ya mjini, halmashauri itawakamata wanyama hao ikiambatana na  utozwaji wa faini kiasi cha shilingi 50,000/= kwa kila mfugo na kila siku ambapo mfugo utakuwa umehifadhiwa, huku ikiuza kwa mnada baada ya siku tano tangu kukamatwa.

Aidha katazo hilo limeendana na sheria ndogo za usafi (Usafi wa Mazingira) za Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, tangazo la serikali NA. 364 la mwaka 2014 pamoja na kanuni za kuondoa adha na usumbufu mijini, (Tangazo la Serikali la Mwaka 2008).