RC Mnyeti mgeni rasmi bonanza la wafanyakazi Manyara

Na John Walter-Babati

Mkuu wa mkoa wa Manyara Alexander mnyeti anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika bonanza la michezo la watumishi wa umma mkoani hapa litakalofanyika oktoba 27 mwaka huu katika uwanja wa Kwaraa mjini Babati. 

Ofisa michezo na utamaduni mkoa wa Manyara Charles Maguzu ambaye ndie mratibu wa bonanza hilo amesema kuwa mpaka sasa maandalizi yanaendelea vizuri na kuweka wazi kuwa lengo ni kujenga afya kwa watumishi kupitia michezo, kujenga undugu,urafiki na mshikamano kwa watumishi wote.

Alisema kwa kutumia  bonanza hilo ambalo limeandaliwa na ofisi ya mkuu wa mkoa wa Manyara wamedhamiria kuhamasisha michezo kwa watumishi wote wa umma ambapo wanataka wafanyakazi wote kutoka halmashauri zote 7 za mkoa huo washiriki.

Alisema michezo itakayochezwa siku hiyo ni mpira wa miguu,netiboli wanawake, wavu,kuvuta kamba,riadha mita 100 na 200,drafi na mchezo wa kunywa soda na mkate ambapo wanawake watashindana kunywa soda pekee na wanaume watashindana kunywa soda na mkate.

Kwa upande wa zawadi alisema washindi watapewa vikombe na kubainisha kuwa kama watajitokeza wadau ambao watasaidia kufanikiza zaidi bonanza hilo basi zawadi zinaweza kubadilika na washindi wakapata fedha na vikombe. 

"Tunatarajia wana michezo 600 kushiriki bonanza letu si mara ya kwanza kufanya kitu kama hiki na itakuwa endelevu niwaombe wadau wa michezo Manyara wajitokeze na kutusapoti katika hili." alisema Maguzu.

Halmashauri zitakazoshiriki katika bonanza hilo ni Simanjiro, Hanang',Kiteto, Babati mji,Babati vijijini, Mbulu mji na Mbulu vijijini.