10/11/2018

Simiyu waboresha ufugaji wa ng'ombe kwa UhimilishajiNa James Timber, Simiyu
Wafugaji Mkoani Simiyu wanatarajia kuboresha ufugaji wao kupitia Mpango Mkakati wa kuboresha ng’ombe wa asili kwa njia ya uhimilishaji kwa lengo la kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao ya mifugo, mpango unaotarajiwa kuanza kutekelezwa mwezi Desemba, 2018.

Hayo yamebainishwa katika kikao cha Wadau wa Mifugo mkoani Simiyu, kilichofanyika Oktoba 10, 2018 mjini Bariadi, kwa lengo la kujadili Utekelezaji wa Mpango mkakati wa kuboresha  mifugo  kwa njia ya Uhimilishaji (Artificial Insermination),chini ya Uenyekiti wa Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka.

Akizungumza katika kikao hicho Mratibu wa Mpango wa Uhimilishaji  kutoka Shirika la Land O’ Lakes, Joachim Balakana amesema  shirika hilo kwa kushirikiana na mkoa wa Simiyu limelenga kuhakikisha wafugaji wa ng’ombe wa kienyeji na kisasa wanafanya uhimilishaji ili kuboresha mbari za ng’ombe wao na kuongeza tija katika uzalishaji wa maziwa na nyama.

“Uhimilishaji utafanyika kwa kutumia mbegu bora zilizozalishwa hapa nchini katika kituo cha Uhimilishaji Arusha, baada ya ng’ombe wa kienyeji kuhimilishwa tunategemea kupata ng’ombe chotara wa waziwa ambao watakuwa wakitoa maziwa mengi na wa nyama watakaofikia uzito mkubwa ndani ya muda mfupi”alisema Balakana.

Ameongeza kuwa kupitia mpango huu ng’ombe zaidi ya 12,000 wanatarajiwa kuhimilishwa mkoani Simiyu kuanzia Desemba, 2018, huku akibanisha kuwa kutokana na mwitikio mkubwa wa wafugaji na viongozi mkoani humo, ng’ombe zaidi ya hao waliolengwa wanaweza kuhimilishwa na ndani ya muda mfupi matokeo makubwa yakaonekana.

Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka amesema mkoa huo una ng’ombe wengi hivyo, uhimilishaji utasaidia kuongeza thamani ya mifugo kwa upatikanaji wa mbegu bora, ambapo ng’ombe wa nyama watakuwa na uzito mkubwa wakiwa na umri mdogo, ngombe wa maziwa kutoa maziwa mengi na ngozi bora pia itapatikana.