https://monetag.com/?ref_id=TTIb Taifa Stars vs Cape Verde, Heshima itue kwa Mbwana Samatta na Erasto Nyoni | Muungwana BLOG

Taifa Stars vs Cape Verde, Heshima itue kwa Mbwana Samatta na Erasto Nyoni


Thom Thomas
Muda mfupi baada ya Taifa Stars kutua nchini, kwa haraka kocha Emanuel Amunike alimuongeza Erasto Nyoni kwenye kikosi. Alitambua nini anakihitaji kutoka kwa Nyoni. Baada ya dakika tisini za leo nadhani ametambua alifanya makosa mwanzo kutolitaja jina la Erasto Nyoni kwenye kikosi.

Erasto Nyoni ni mchezaji anayekupa option nyingi uwanjani. Anaweza kucheza nafasi yeyoye uwanjani. Pia ni mchezaji mzoefu, ameichezea Taifa Stars kwa zaidi ya miaka kumi sasa.

Leo alicheza zaidi kama kiungo mkabaji. Alikua bora sana. Alitawala eneo lote la kiungo, Taifa Stars ilicheza kupita yeye. Ni yeye aliyeanzisha mashambulizi, ni yeye aliyeiongoza safu ya Ulinzi huku akiwaongoza vyema viungo Himid Mao na Mudathiri Yahya pia.

Kazi ya Himid Mao ilikua ni kukaba. Kwa sasa nchini Tanzania hakuna kiungo halisi anayejua nini maana ya kukaba kama Himid Mao. Alikimbia kila sehemu ya uwanja akikaba na kutafuta mpira. Kazi ambayo amekua akiifanya kwa ubora siku zote.

Alichokua anakofanya Mudathiri Yahya ni kiunganisha safu ya kiungo na ile ya ushambuliaji. Alicheza kama kiungo mchezesha-timu. Pasi ya goli la pili aliyompatia Mbwana Samata huku kwetu huwa tunaiita 'pasi ya hela'. Ingeshangaza kuona Samata akikosa goli.

Idara ya ulinzi iliongozwa na Kelvin Yondani na Aggrey Morris. Hawa ni watu wa kazi. Tangu nimeanza kuwafahamu wamekua katika kiwango bora siku zote. Umakini, nguvu, akili na uzoefu wao alifanya ngome ya ulinzi iwe ngumu zaidi. Washambuliaji wao, Ricardo Gomes, Garry Rodriguez na Djaniny wote hawakuwa na madhara.

Mbwana Samata 'champion boy'. Hakika huyu ndiye mchezaji staa na muhimu zaidi kwenye kikosi cha Taifa Stars. Alichokifanya ni kutoa kile alichotakiwa kukitoa. Alifanya kile ambacho alitakiwa kukifanya. Alikua kila kitu kwenye eneo la ushambuliaji. Ukimuongeza na Simon Msuva, Taifa Stars ikawa hatari sana hasa namna ambayo walikua wakitengeneza mashambulizi.

Baada ya kukosa penati, alitambua mzigo mkubwa umebaki kwake. Taifa Stars ilihitaji zaidi kupata matokeo. Kitu kizuri ni kwamba hata baada ya kukosa penati hakuwa na presha, alitambua anaweza kufanya zaidi. Akafanya. Goli moja na assist moja kutoka Mbwana Samata. Nini kingine umakitaji kutoka kwake?

Wakati sisi tukiwa na Mbwana Samata kama mchezaji staa kwenye kikosi, Cape Verde wao walikua na staa wao, Garry Rodrigues. Huyu ni mmoja kati ya wachezaji muhimu kwenye kikosi cha Galatasaray nchini Uturuki. Alikua kila kitu kwa Cape Verde.

Timu nzima ilicheza ikimuangalia yeye. Mpira ulipokua mguuni mwake mabeki wa Taifa Stars walipata shida kuupata. Bahati mbaya mara nyingi alikutana na Shomari Kapombe, Aggrey Morris na Kelvin Yondani. Akazimwa, kashindwa kuleta madhara.

Approach ya Amunike ilikua nzuri sana. Alichokifanya ni kutengeneza umakini hasa kwenye kuzuia mashambulizi na kutengeneza umakini eneo la ushambuliaji. Hakuhitaji kushindana na Cape Verde kwenye kumiliki mpira. Ndio maana aliamua kuanza na Abdi Bands pamoja na Gadiel Michael upande wa kushoto, huku Himid Mao akimsaidia Kapombe upande wa kulia.

Feisal Salum 'Fei Toto'. Wakati mwingine ni vyema kama tutashukuru ujio wake Tanzania bara, yawezekana kama angeendelea kuwepo visiwani Zanzibar tusingefahamu nini anaweza kukifanya.

Fei Toto ana kipaji halisi. Anajua ni wakati gani anatakiwa kakaba, wakati gani anatakiwa kucheza timu na ni wakati gani anatakiwa kutoa burudani ya soka. Ni kiungo fundi anayejua nini anachotakiwa kukifanya. Baada ya kuingia uwanjani ilikua ni burudani sana kumtaza akicheza.

Matokeo ni 2-0. Baada ya matokeo haya ni wazi bado tuna nafasi ya kwenda Cameron. Kwa sasa maombi yetu ni kwa Uganda. Kinachotakiwa ni kuomba Uganda ashinde mechi zake dhidi ya Lesotho na Cape Verde. Baada ya hapo kazi itabaki kwetu kumalizana na Uganda uwanja na taifa na kutafuta matokeo ugenini dhidi ya Lesotho.

Taifa Stars kwanza.

0754 896963