Wakuu wa Umoja wa Ulaya kuitisha mkutano wa kuagana na Uingereza


Viongozi wa Umoja wa Ulaya wameamua kuuweka kando mpango wao wa kuitisha mkutano maalum juu ya mkataba wa kupeana talaka na Uingereza uliokuwa umepangwa kufanyika katikati ya mwezi ujao.

Mjumbe mkuu wa Umoja wa Ulaya kwenye mazungunzo na Uingereza Michel Barnier amesema pande hizo mbili  zinahitaji muda zaidi. Barnier amesema muda zaidi unahitajka ili kuweza kupiga hatua muhimu.

Kwenye mkutano wao wa siku ya Jumatano viongozi wa Umoja wa Ulaya walisema, licha ya kufanyika mazungumzo ya kina, hatua kubwa haijafikiwa ya kuwezesha kufanyika mkutano maalumu uliokuwa umepangiwa tarehe 17 na 18 mwezi ujao wa Novemba.

Wakuu wa nchi na serikali wa Umoja wa Ulaya wamesema wataitisha mkutano wa kilele ili kuukamilisha mkataba wa kuagana na Uingereza endapo utaonekana uwezekano wa makubaliano kufikiwa.