Waziri Mkuu atoa onyo kwa watumishi wa umma, " Hatutovumilia wadokozi wa mali"


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema vitendo vya udokozi wa mali ya umma havitavumiliwa na Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli, hivyo amewataka watumishi wawe waadilifu na waaminifu wanapotekeleza majukumu yao.

Ameyasema hayo leo (Alhamisi, Oktoba 11, 2018) wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa katika mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa halmashauri hiyo akiwa katika ziara mkoani Dodoma.

Waziri Mkuu amesema Serikali haitamvumilia watumishi wa umma ambaye si muadilifu, mvivu na wala rushwa hawana nafasi, hivyo ni lazima wajibike na ambao watashindwa kutekeleza majukumu yao watapa shida kwenye Serikali hii. “Hakuna mchezo kwenye Serikali hii, watumishi wa umma wanapaswa kulitambua hili.”

Hata hivyo, Waziri Mkuu amewataka watumishi hao kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa kufuata maelekezo yaliyotolewa kwenye Ilani ya uchaguzi Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya 2015/2020.

Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka watumishi hao wahakikishe wanapanga ratiba ya kwenda kuwatembelea wananchi hususani waishio vijijini na kushirikiana nao katika kutatua kero zinazowakabili si kukaa ofisni.

Waziri Mkuu amesema kila mtumishi kwenye idara yake anapaswa kwenda kwa wananchi, kama ana siku tano za kufanya kazi kwa wiki basi siku tatu azitumie kwenda kwa wananchi kutatua changamoto zao na kama ana siku sita, siku nne azitumie kuwafikia wananchi.

Akizungumzia kuhusu idara ya kilimo, Waziri Mkuu amesema Maafisa Kilimo wote wanatakiwa kwenda vijijini kufanya kazi na si kubaki ofisini na alishatoa agizo hilo alipokutana nao jijini Dodoma. “Wakulima huko vijijini wanahangaika peke yao huku maafisa kilimo wamekaa ofisini.”

Waziri Mkuu amewataka watumishi wa umma wazingatie itifaki, mipaka ya madaraka yao pamoja na kuheshimu viongozi. Amesema hata kama ni mkuu wa idara pia anapaswa kumheshimu mtumishi aliyekuwa chini yake.