https://monetag.com/?ref_id=TTIb Baada ya ujio wa Jeshi Usu, Naibu Waziri awatoa hofu watumishi juu ya maslahi yao | Muungwana BLOG

Baada ya ujio wa Jeshi Usu, Naibu Waziri awatoa hofu watumishi juu ya maslahi yao

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu ( wa kwanza kushoto) akiwa ameongozana na Menejimenti ya Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro akipewa maelezo wakati alipotembelea jana kabla ya kuzungumza na kuwasikiliza watumishi wa Mamlaka hiyo juu ya changamoto mbalimbali zinazowakabili ili kuweza kuzitafutia ufumbuzi
Naibu Waziri Wizara ya  Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu amewatoa hofu watumishi wa Taasisi zenye jukumu la kulinda na kuhifadhi Wanyamapori na Misitu nchini kuwa hakuna maslahi yao yatakayobadilika baada ya ujio wa Jeshi Usu

Naibu Waziri Kanyasu ameyasema hayo wakati akizungumza na watumishi wa Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro ikiwa ni mara yake ya kwanza  kukutana na watumishi hao tangu alipoteuliwa  kushika wadhifa wa Naibu Waziri katika Wizara hiyo  nyeti kwa uchumi wa nchi.

Amesema ziara yake imelenga kuzifahamu Taasisi  anazoziongoza ili kujua namna zinavyotenda kazi na  changamoto zinazowakabili ili kuzipatia ufumbuzi.

Akizungumza kuhusu utendaji wa Jeshi USU, Naibu Waziri Kanyasu amesema kufuatia mabadiliko ya mfumo wa utendaji kutoka katika mfumo wa kiraia na kuwa Jeshi USU kutakuwa na mabadiliko kiutendaji yatakayoendana na taratibu za Jeshi USU lakini utakaoheshimu na kulinda maslahi ya watumishi.

Naibu Waziri huyo ameeleza kuwa, uanzishwaji wa Jeshi hilo haukusudii kubadili maslahi ya watumishi hao  na endapo maslahi hayo yatabadilika basi yatakuwa na mabadiliko chanya kwao.

Naibu Waziri Kanyasu ameongeza kuwa Jeshi USU litaongeza nidhamu uwajibikaji na maadili kwa watumishi wa sekta ya Maliasili na  Utalii ili waweze kusimamia ipasavyo uhifadhi endelevu wa maliasili na si vinginevyo.

Katika hatua nyingine,  Naibu Waziri Kanyasu ameiagiza Menejimenti ya Mamlaka ya  Hifadhi ya eneo la Ngorongoro ibuni  vivutio  vipya vya  Utalii vitakavyosaidia  kuongeza  mapato kwa Serikali kwa kuzingatia majukumu makuu ya Taasisi.

Kwa upande wake, Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro, Freddy Manongi amewahakikishia  watumishi hao  kuwa maslahi yao hayatabadilika na ikiwezekana yataongezwa kwa sababu uwajibikaji utaongezeka baada ya ujio wa Jeshi Usu

Ameongeza kuwa mfumo wa Jeshi Usu haumaanishi kuwa Watumishi hawapaswi kupewa maslahi yao na badala yake yanahitaji kuboreshwa zaidi ili waweze kuwa  na ari ya kufanya kazi katika kulinda Wanyamapori na Misitu nchini.

”Kati ya masuala ambayo nayapigania yasiweze kubadilika baada ya ujio wa Jeshi Usu ni maslahi yenu” amesema Dkt. Manongi.

Jeshi USU  lilizinduziwa rasmi  tarehe 17 Novemba mwaka huu na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan katika Uwanja wa Fort Ikoma  wilayani Serengeti  mkoa wa Mara.