DC Arusha apata msaada kutoka Shirika la Friends of German

Na Elinipa Lupembe, Arusha

Shirika lisilo la kiserikali la Help for Maasai Childreni (HMC), kwa kushirikiana na wafadhili wa Kundi la Friends of German la nchini Ujerumani, limetoa msaada wa magari matano katika halmashauri ya Arusha wilayani Arumeru kwa lengo la kutatua changamoto zinazoikabili jamii hususani magari ya kubebea wagonjwa.

Akipokea msaada huo Mkuu wa wilaya ya Arumeru Mhe. Jerry Muro amewashukuru wafadhili hao kwa msaada  wenye tija kwa wananchi wa halmashauri ya Arusha na wilaya ya Arumeru kwa ujumla wake huku  akimpongeza Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo  Dkt. Wilson Mahera  kwa kushirikiana vyema na Taasisi hizo kwa kuweza kuchangishana fedha za kununua magari hayo kutoka nchini Ujerumani na  hatimaye  kuwafikia wananchi wa Arumeru.

Aidha Mkuu huyo wa Wilaya amepongeza juhudi kubwa, zinazoendelea kufanywa na Taasisi hizo, katika kutekeleza miradi ya huduma za jamii katika, sekta nyeti za  Elimu, Afya na Maji, na kuwawezesha wananchi wa Oldonyowas kupata huduma muhimu ndani ya eneo lao ambapo hapo awali ilikuwa inawawia ugumu kupata huduma  hizo kwa wepesi.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Arusha Dkt. Wilson Mahera, amewaelezea wafadhili hao  kuwa waliingia hapa nchini mwaka 2005, na wamekuwa wakifadhili utekelezaji wa miradi ya maji, elimu na afya kwenye kata za Oldonyosambu na Oldonyowasi.

Amefafanua kuwa halmashauri hiyo, imepokea jumla ya magari matano, kati ya hayo, magari mawili ni ya kubeba wagonjwa 'Ambulance' ambayo ni 'mobile clinic' yakiwa na vifaa muhimu vya kuweza, kufanyia mgonjwa upasuaji ndani ya gari, na kuongeza kuwa magari matatu aina ya 'Pick up' yatatumika kwa shughuli mbalimbali ndani ya halmashauri hiyo.

Hata hivyo alieleza kuwa, mwaka 2009, wafadhilia hao walitekeleza mradi wa Afya kwa kujenga Zahanati ya kisasa katika kata ya Oldoyowasi, ambayo imejitosheleza kwa vifaa tiba, Zahanati ambayo imewapunguzia adha wananchi wa Oldonyowas ya kutembea umbali mrefu kutafuta huduma ya afya.

Dkt. Mahera amesisitiza kuwa, wafadhili hao ni muhimu kwa halmshauri yake, kwa kuwa tayari wamejenga jumla ya shule saba za awali sambamba na kuwapeleka waalimu kwenye mafunzo ya ualimu kwa lengo la kufundisha watoto wa madarasa hayo ya awali.

Mkurugenzi wa shirika la Help for Masaai Childreni, Joseph Kivuyo licha ya kushukuru kwa msaada huo, ameeleza kuwa, lengo la kutolewa magari hayo ni kurahisisha kutoa huduma kwa wananchi waishio katika maeneo yenye mazingira magumu hususani vijijini.

“Tuliamua kuchanga fedha za kununua magari haya kutokana na jamii inayotuzunguka kuwa na uhitaji mkubwa wa uhudama hii hasa wanawake ambao mara nyingi ndiyo waliokuwa wakitembea umbali wa kilomita 18 kwenda kwenye vituo vya mbali kutafuta huduma,” amesema Kivuyo.

Naye kiongozi wa kundi la Friends of German, ambaye ndiye mfadhili aliyechangisha fedha za kununua magari hayo, Harld Ppeiffer, amesema kuwa, miaka kumi iliyopita alipata wazo la kuja katika nchi za bara la Afrika kwa ajili ya kusaidia watoto kupata elimu.

Amedai kuwa, kutoa elimu bora kwa watoto ni jambo muhimu sana, kwa sababu itawafanya kuwa na malengo mazuri kwa maisha yao ya baadae na kuongeza kuwa,  msaada huo wa magari ni muhimu katika kutimiza wazo lake la kuwasaidia watoto wa Afrika hasa nchini Tanzania na watoto wa kata ya Oldonyowas.

Wakifurahia msaada wa magari hayo wananchi wa kata ya Oldonyowas ambao ndio wanufaika wa magari hayo walionyesha kushindwa kuficha hisia zao wakionyesha furaha kwa  kucheza na kuimba, mara baada ya magari hayo kuwasili katika halmashauri hiyo.