https://monetag.com/?ref_id=TTIb FA yakata rufaa dhidi ya Mourinho | Muungwana BLOG

FA yakata rufaa dhidi ya Mourinho

Chama cha soka England, FA, kimeamua kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa kutomshtaki meneja wa Manchester United Jose Mourinho kutokana na maneno aliyoyasema baada ya mechi.

FA wanadai kwamba Mourinho alitumia lugha ya matusi kwa lugha ya Kireno, akizungumza kwenye kamera ya televisheni, alipokuwa anaondoka uwanjani baada yao kushinda mechi dhidi ya Newcastle 3-2 mnamo 6 Oktoba.

Hata hivyo, United walifanikiwa kupinga mashtaka hayo.

Rufaa ya FA imetokea baada yao kukutana na kutathmini sababu zilizokuwa zimetolewa na Tume Huru ya Usimamizi inayoangazia masuala ya soka, kwa njia ya maandishi.

Shirikisho hilo linalosimamia soka Uingereza lilieleza kushangazwa kwake na uamuzi wa tume hiyo wa kumuondolea hatia Mourinho, uamuzi ulioanywa na jopo la watu watatu.

Jopo hilo lilifikia uamuzi huo baada ya kumtumia mtaalamu wa kusoma midomo ya mtu kubaini anasema nini.

FA ilishangazwa na hatua hiyo kwani mtaalamu huyo aliunga mkono mashtaka kwamba meneja huyo kutoka Ureno alitumia lugha ya kuudhi.

Lakini BBC imefahamu kwamba United waliwasilisha hoja zenye uzito kumtetea meneja wao, na kwamba walikuwa wameamini kwamba uamuzi wa jopo hilo uliwaondolea makosa.

Mourinho anaonekana kwenye kamera ya TV akisema jambo, kisha kutoa ishara kwa mkono wake wa kulia alipokuwa akiondoka uwanjani baada ya timu yake kutoka nyuma na kuwalaza Newcastle.

Mourinho huenda akapigwa marufuku kutokuwepo uwanjani wakati wa mechi kwa muda iwapo atapatikana na hatia.