Jinsi ya kuwa na muonekano wa urembo siku zote


Dhana ya urembo imekuwa na tafsiri tofauti kwa watu wengi. Kila mmoja anautafakari urembo kwa namna yake kulingana na malezi na mahali alipo. Wako wanaoamini kuwa mrembo ni lazima uwe na ngozi nyeupe, wengine hudhani kuwa ili kuonekana mrembo, lazima uwe na nywele ndefu, lakini pia wapo wanaodhani kwamba ili uwe mrembo ni lazima uwe na umbo namba nane.

Hiyo yote ni mitazamo tu, lakini tafsiri halisi kutoka kwa wataalamu wa urembo ni kwamba; urembo ni hali ya kuwa na afya bora.

Kama ni hivyo, kipi kifanyike ili uwe mrembo?

Kabla hujafanya chochote kuhusu afya yako, unatakiwa kuamini kwamba wewe ni mrembo. Ikiwa utasimama katika hilo ni kweli utakuwa mrembo siku zote...


Safisha ngozi yako

Hakikisha ngozi yako inakuwa safi muda wote. Unaweza kutumia njia mbalimbali kama vile kuondoa ngozi zilizokufa mara kwa mara. Kuondoa mafuta yaliyogandamana katika ngozi kwa kufanyia masaji ngozi yako ili kurahisisha mzunguko wa damu yako.

Ikiwa hili litafanyika kwa umakini ni wazi kuwa matatizo ya kuwa na chunusi au weusi katika ngozi yako havitakuwepo kwako.

Tumia bidhaa za nywele, ambazo zinaendana na nywele zako na hakikisha unazingatia mambo muhimu katika uboreshaji wa nywele zako. Miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na kutokutumia vifaa vinavyounguza nywele. Epuka kuosha nywele kwa maji ya moto, pia kuchana nywele zikiwa na maji, kwani unaweza kusababisha kukatika kwa nywele zako.

Safisha meno yako: Usafi wa meno pia ni miongoni mwa mambo ya kuzingatia unapoamua kuboresha urembo wako. Hakikisha unapiga mswaki walau mara mbili kwa siku kila siku au kila baada ya kula.

Usipake vipodozi mara kwa mara: Tumia vipodozi pale inapobidi, usipendelee kutumia vipodozi mara kwa mara kwani wakati mwingine matumizi ya mara kwa mara ya vipodozi, husababisha madhara katika ngozi yako, hasa unapotumia bila kufuata maelekezo ya wataalamu.

Fanya mazoezi: Hakikisha mazoezi yanakuwa sehemu ya maisha yako, hii itasaidia kukufanya uonekane siyo tu mrembo, bali pia mwenye kujiamini.

Pata usingizi wa kutosha: Hakikisha unapata usingizi wa kutosha kila siku. Kwa mujibu wa wataalamu, unatakiwa kulala si chini ya saa nane kila siku. Ikiwa utapata usingizi wa kutosha ni wazi kuwa macho yako yataonekana yenye nuru siku zote. Pia utazidi kuonekana kuwa mrembo zaidi.