Mbunge ambana Waziri kuhusu kauli ya Rais Magufuli "Fyatueni"



Mbunge wa Viti Maalum (CHADEMA) , Suzan Lymo ameomba ufafanuzi wa kauli iliyotolewa na Rais Dkt John Pombe Magufuli ambayo iliwataka wananchi kuendelea kutopangiwa idadi ya watoto bali wajichagulie wenyewe.

Lyimo ameuliza swali hilo kwa Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Dkt Faustine Ndugulile alidai anapata mkanganyiko afutae kauli ipi kati ya kauli ya Rais Magufuli au sera ya uzazi wa mpango.

Akijibu swali hilo, Dkt. Ndugulile amesema serikali haijatoa tamko la kusitisha huduma ya uzazi wa mpango bali Rais Magufuli alitaka watu wazae kulingana na uwezo wao.

“Sisi kama serikali hatujaweka ukomo wa idadi ya watoto mwananchi anatakiwa kuzaa, tunachosisitiza sisi kama serikali tunasema mtu awe na idadi ya watoto anaoweza kuwamudu na kuwatunza na huo ndio msisitizo wetu , Kwahiyo sisi kama serikali hatujatoa tamko la kusitisha huduma ya uzazi wa mpango hiyo barua haipo na haita kuwepo, alichosema Rais mtu anakuwa na idadi ya watoto ambao ataweza kuwatunza.”

Agosti 12 mwaka 2016 akiwa Jijini Dar es salaam Rais Magufuli alisema “darasa la kwanza kwa mwaka huu wamefika milioni 2, nataka niwaeleze watani wangu wa Dar es salaam ni kuzaa tu, fyatua mtoto wako atasoma bure la kwanza mpaka sekondari.”