11/08/2018

Okwi anyakua tuzo ya mchezaji bora TPL

Mshambuliaji Emmanuel Okwi wa klabu ya Simba achaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Oktoba wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) msimu wa 2018/2019.

Okwi amenyakua tuzo hiyo baada ya kuwashinda wenzake wawili, Yahya Zayd wa Azam na Eliud Ambokile wa Mbeya City alioingia nao fainali katika uchambuzi uliofanywa Dar es Salaam wiki hii na Kamati ya Tuzo ya TPL inayotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kutokana na mapendekezo ya makocha waliopo viwanja mbalimbali ambavyo ligi hiyo inachezwa msimu huu.

Okwi raia wa Uganda ameweza kutoa msaada mkubwa kwa klabu yake ya simba na kuiwezesha kupata pointi 12  kwa kushinda michezo yote na kumaliza ikiwa nafasi ya pili, huku Okwi akifunga mabao 7 kwa mwezi huo, matatu akifunga katika mchezo dhidi ya Ruvu Shooting ambao Simba iliibuka na ushindi wa mabao 5-0.

Ambokile naye alitoa mchango mkubwa kwa Mbeya City na kuiwezesha kupata pointi 11 baada ya kushinda michezo mitatu na kutoka sare michezo miwili na kushika nafasi ya nane katika msimamo, akifunga mabao manne.

 Kuhusu Zayd alitoa mchango mkubwa kwa Azam akifunga mabao matatu katika michezo mitano ambayo Azam ilicheza ikishinda yote na kupata pointi 15 ikishika nafasi ya kwanza.