RC Mwanri: Mkoa wa Tabora unakwenda Jerusalem mpya


Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri amesema kama mkoa huo hautapata maendeleo ya kiuchumi wakati huu wa Serikali ya AwamuTano basi usahau habari ya maendeleo.

Mwanri amesema mjini Tabora kuwa, Haiwezekani mkoa huo wenye sifa kubwa kihistoria ukabaki masikini, na kwamba, watu mkoani humo wakiendelea kuishi maisha duni wa kulaumiwa si wananchi bali viongozi kwa kuwa watakuwa wameshindwa kuwaonyesha njia.

"Tusikae hapa tunaabudu mambo ya ajabu ajabu, mambo ya ushirikina tuachane nayo, tumfuate Mungu, tumtafute Mungu alipo, tusiamini ubinadamu tu, Tabora we can, tunaweza."

Tabora, Tabora, Tabora sisi tunaweza, tuna akili, maprofesa wakubwa walitoka Sikonge, walioongoza nchi, wanaoongoza nchi wote walisoma Tabora,"amesema Mwanri na kuongeza kuwa, mkoa huo unakwenda Jerusalem mpya, nchi ya ahadi yenye asali na maziwa.

Amesema, hakuna mwanadamu asiye na akili, na kwamba, tofauti ya akili baina ya watu ipo kwenye matumizi tu.

Aidha amewataka wananchi wa Tabora wabadilike kifikra na waamini kwamba wanaweza kupata mafanikio kiuchumi na watambue kwamba, fursa hazitolewi, zinachukuliwa.

"Na leo nataka niiambie Tabora yes we can na itakuwa, semeni yes we can, semeni yes we can, ndio tunaweza, Tabora nina uhakika kwamba tunaweza Tabora, Tabora ni taa bora," amesema Mwanri wakati wa mkutano wa wadau wa Jukwaa la Fursa za Biashara Tabora linalotarajiwa kufanyika Novemba 21 hadi 23 mjini Tabora.