Serikali yataja fedha iliyotoa kuimarisha elimu kwa kipindi cha mwezi Julai hadi Oktoba



Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kati ya Julai na Oktoba, mwaka huu, Serikali imetoa jumla ya sh. bilioni 83.2 ili kuimarisha usimamizi na uendeshaji wa shule nchini.

Waziri Mkuu amesema, kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 38.6 zilipelekwa kwenye shule za msingi na shilingi bilioni 44.6 zilienda kwenye shule za sekondari ikiwa ni utekelezaji wa mpango wa elimumsingi bila malipo.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo Novemba 16, 2018 bungeni mjini Dodoma wakati akitoa hoja ya kuahirisha mkutano wa 13 wa Bunge. Bunge limeahirishwa hadi Januari 29, 2019.

“Katika kuimarisha usimamizi na uendeshaji wa shule nchini, Serikali inapeleka fedha za elimumsingi bila malipo moja kwa moja shuleni. Kwa mfano, katika kipindi cha Julai hadi Oktoba, 2018 shilingi bilioni 38.6 zilipelekwa katika shule za msingi na shilingi bilioni 44.6 kwenye shule za sekondari,” amesema.

Amesema tangu kuanza kutekelezwa kwa mpango wa elimumsingi bila malipo, uandikishaji wa watoto wa darasa la awali na darasa la kwanza umeimarika na kwamba kumekuwepo na mwenendo mzuri wa ufaulu kwenye mitihani ya kumaliza darasa la saba.

“Kumekuwepo na mwenendo mzuri wa ufaulu katika mitihani ya kumaliza darasa la saba, ambapo mwaka 2016 ilikuwa wastani wa asilimia 70 na mwaka 2018 ilikuwa ni wastani wa asilimia 78. Hali hiyo, imeongeza mahitaji mbalimbali, ikiwemo miundombinu katika shule zetu za msingi na sekondari,” amesema.

Waziri Mkuu amesema katika kukabiliana na hali hiyo, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa elimu inaendelea na mikakati ya ujenzi na ukamilishaji wa miundombinu muhimu ya shule.