Serikali yawapongeza wananchi kwa kujenga shule

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua ujenzi wa Shule ya Msingi ya kwenye kijiji cha Kilimahewa unaofanywa na wananchi  wa Kata ya Nachingwea wilayani Ruangwa, Novemba 20, 2018

Waziri Mkuu,  Kassim Majaliwa amewapongeza wakazi wa kata ya Nachingwea wilayani Ruangwa kwa kujenga shule ya msingi  kwenye kijiji cha Kilimahewa.

“Uamuzi wa kujenga shule ya msingi ni sahihi kwa kuwa huwapunguzia watoto kutembea umbali mrefu na pia utarahisisha mazingira ya kusomea kwa watoto wetu.”

Waziri Mkuu ametoa pongezi hizo leo (Jumanne, Novemba 20, 2018) alipotembelea eneo la ujenzi wa shule ya msingi Lugalo na kuwataka waendelee na moyo huo.

Amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli inataka kila mtoto aliyefikia umri wa kwenda shule aanzishwe shule na asome.

Kadhalika, Waziri Mkuu ametaka wananchi hao waweke pembeni itikadi zao za kisiasa na badala yake washirikiane kujenga miradi ya maendeleo kwenye eneo lao.

Naye, Mtendaji wa Kijiji cha Kilimahewa, Majuto Ungulu amesema ujenzi wa shule hiyo uliibuliwa na wakazi wa kijiji hicho, ambacho hakina shule ya msingi.

Majuto amesema watoto wa kijiji hicho wanalazimika kutembea umbali wa kilomita mbili hadi shule la msingi Ruangwa, hivyo ujenzi huo utawawezesha kusoma karibu.

Amesema kwa sasa wameanzia na ujenzi wa vyumba vinane vya madarasa, matundu 18 ya vyoo na ofisi mbili za walimu ambapo jumla yake ni sh. milioni 399.8.