Ufahamu kiundani ugonjwa wa tezi dume.

Moja ya maradhi yanayoshuhudia kampeni kubwa kukabiliana nayo katika miaka ya hivi karibuni duniani ni pamoja na saratani ya tezi dume kutokana na ukubwa wa athari inazosababisha.

Ni maradhi yanayoshika nafasi ya tatu kwa kusababisha vifo vinavyotokana na saratani kwa wanaume duniani.

Pia ni chanzo kikuu cha vifo vinavyosababishwa na saratani kwa wanaume wenye umri wa miaka 70 na kuendelea.

Hata hivyo, satarani ya tezi dume kwa sasa inawapata zaidi wanaume kuanzia miaka 25.

Maana ya saratani
Saratani maana yake ni ukuaji holela bila mpangilio wa seli baada ya kuparanganyika kwa mfumo wa seli unaodhibiti ukuaji na uhai wake. Na uvimbe wa kawaida wa tezi maana yake ni kuwa seli zimetutumka tu lakini hakuna mparanganyiko wa seli wala kukua kwa kusambaa kiholela kama ilivyo kwa saratani.

Hivyo, ndio maana kuna tatizo la kuvimba tezi dume na wengine kupata saratani ya tezi dume kwa wanaume wenye umri mkubwa.

Tezi dume ni sehemu mojawapo ya mfumo wa uzazi wa kiume. Inaundwa na sehemu mbili ambazo zimeunganishwa na kufunikwa kwa nje kwa utando wa tishu.

Tezi hii ipo mbele kidogo ya puru (rectum) na chini kidogo ya kibofu cha mkojo. Tezi dume inauzunguka mrija unaounganisha kibofu cha mkojo na uume (urethra).

Kazi ya tezi dume
Mojawapo ya kazi za tezi dume ni kutoa majimaji yanayochanganyika na mbegu za kiume (sperms) wakati wa kilele cha tendo la kujamiana. Mchanganyiko huu wa mbegu pamoja na majimaji hayo hutengeneza shahawa (semen).

Majimaji hayo husaidia kuzipa mbegu za kiume nguvu ya kusafiri kwenye uke mpaka kufikia kwenye mirija ya uzazi, tayari kwa utungisho na yai la kike.

Vilevile husaidia kupunguza hali ya kitindikali iliyopo katika uke, ambayo isiporekebishwa, huua mbegu nyingi za kiume na kufanya utungisho kuwa wa tabu..

Vyanzo Vinavyopelekea Tezi Dume Kutanuka:
Tatizo la kutanuka kwa tezi dume limekuwa kwa kasi sana hii ni kutokana na mitindo ya maisha wanaume wengi wanayoishi. Pia na elimu ndogo iliyoko kwenye jamii kuhusu afya zao.

Vifuatavyo ni vyanzo vya kutanuka kwa tezi dume:
  • Ukosefu wa lishe kamili na Virutubisho muhimu mwilini.
  • Uwepo wa sumu nyingi mwilini.
  • Kutokufanya mazoezi.
  • Matumizi ya pombe kali, na uvutaji wa sigara.
  • Uzito mkubwa (uliopindukia, uliokithiri), na Kitambi.
  • Kutokukaa sawa kwa vichocheo vya mwili (Hormone Imbalance).
  • Msongo wa mawazo (Stress).
  • Magonjwa ya zinaa.
  • Umri mkubwa.
  •  Upasuaji wa korodani, kuzaliwa na korodani moja.
  • Historia ya Familia (Kurithi).
  • Mazingira (Ethnicity).
 
Dalili za saratani ya tezi dume ni zipi?

a) Dalili za awali
  • Kukojoa mkojo uliochanganyikana na damu
  •  Kukojoa mkojo wenye mtiririko dhaifu
  • Maumivu kwenye mfumo wa mkojo
  • Kuhisi maumivu wakati wa kukojoa
  • Kuhisi kibofu kimeja mkojo muda wote na ukienda kukojoa mkojo hautoki, lakini ukirudi kukaa unahisi kukojoa tena.
  • Homa
Kukojoa mara kwa mara wakati wa usiku

b) Dalili za mtu aliyeathirika


  • Maumivu ya mifupa hasa chini ya mgongo, kiuno na mbavu
  • Miguu kuwa dhaifu
  • Kushindwa kumudu tendo la ndoa, au Kuhisi maumivu makali wakati unamaliza tendo la ndoa.
  • Kushindwa kuzuia mkojo, pindi unapohisi kukojoa
  • Kushindwa kuzuia haja kubwa (kinyesi cha maji maji)
  • Tumbo kujaa gesi mara kwa mara
 
 
Vipimo gani vitathibitisha kuwa nina saratani ya tezi dume?
Utambuzi wa saratani ya tezi dume hujumuisha kufahamu historia ya mgonjwa pamoja na familia yake, kufahamu dalili alizo nazo mgonjwa pamoja na kufanya vipimo kadhaa. Vipimo vinavyoweza kufanywa ni pamoja na
 
Digital rectal exam: Daktari ataingiza kidole cha shahada katika puru (rectum) ili kuhisi tezi dume kupitia ukuta wa puru. Aidha atahisi pia sehemu zote 

zinazozunguka tezi dume kutambua iwapo tezi ni ngumu au kama ina uvimbe wowote.
 Kipimo cha damu kuchunguza Prostate Specific Antigen (PSA): PSA ni aina ya protein inayozalishwa na seli za tezi dume. Uzalishaji wake huongezeka wakati wa BPH, tezi dume inapopata uambukizi (prostitis) , na saratani ya tezi dume. DRE pamoja na PSA huonesha uwepo wa tatizo kwenye tezi dume lakini vipimo hivi havina uwezo wa kutofautisha iwapo tatizo hilo linamaanisha saratani au BPH. Hivyo basi, ili kuweza kutofautisha kati ya magonjwa hayo mawili, kipimo kiitwacho Prostate biopsy hufanywa.
Prostate biopsy: Kipimo hiki hufanywa kwa kuchukua kipande cha nyama (tishu) kutoka tezi dume kwa ajili ya uchunguzi maabara.
Kipimo kingine huitwa transrectal ultrasound ambacho husaidia kuonesha ukubwa na sura ya tezi dume lilivyo.
 
Ili kutambua kama saratani imesambaa sehemu nyingine za mwili vipimo vya CT scan, MRI pamoja na PET navyo vyaweza kufanyika pia.

Madhara ya Tezi Dume:
Yafuatayo ni madhara ya tezi iliyotanuka:


  • Kibofu cha mkojo kuuma: hivyo hupelekea mkojo kurudi juu, na kuharibu figo na Ini … … n.k.
  •  Kufunga kwa njia ya mkojo kabisa
  • Figo kushindwa kufanya kazi (Kidney Failure)
  •  Kushindwa kumudu tendo la ndoa (Ndoa zinavunjika)
  •  Ugumba (Infertility, Frigidity for men)
  •  Kutokea kwa majipu sehemu ya Tezi Dume
  • Kifo
 
Saratani ya tezi dume inatibika?
Ndiyo! Kuna njia kadhaa za matibabu ya saratani ya tezi dume. Hata hivyo uamuzi wa njia gani itumike unategemea ushauri na maoni ya daktari kulingana na hatua ya ugonjwa ulipofikia na umri wa mgonjwa husika.
 
Katika hatua za awali za ugonjwa, daktari anaweza kushauri mgonjwa atibiwe kwa kufanyiwa upasuaji na tiba ya mionzi, wakati kwa wagonjwa wazee, daktari anaweza kushauri kumfuatilia mgonjwa kwa ukaribu bila kumfanyia upasuaji au bila kumpatia tiba ya mionzi.
 
Iwapo saratani imesambaa na kuathiri sehemu nyingine za mwili, matibabu yake yanaweza kujumuisha upasuaji wa kuondoa korodani, matumizi ya dawa za kupunguza kiwango cha homoni ya testosterone katika damu (hormonal therapy), au matumizi ya kemikali za kuua seli za saratani (chemotherapy).
 
Upasuaji

Upasuaji hufanyika kwa wagonjwa walio katika hatua za awali za ugonjwa (stage I na stage II) ingawa pia hufanywa kwa baadhi ya wagonjwa walio katika hatua za mwisho za ugonjwa huu yaani stage III na stage IV. Upasuaji unaofanywa ni ule wa kuondoa tezi dume pamoja na baadhi ya tishu zinazozunguka tezi hiyo.
 
Tiba ya Mionzi
Hii ni aina ya tiba inayotumia mionzi kuua seli zenye saratani. Tiba ya mionzi hutumika kutibu saratani ya tezi dume ambayo haijasambaa kwenye sehemu nyingine za mwili. Aidha inaweza pia kutumika kuua masalia ya tishu zenye saratani mara baada ya kufanyika kwa upasuaji.
 
Kwa wagonjwa walio katika hatua ya mwisho ya saratani yaani wale ambao saratani tayari imeshasambaa mwilini, mionzi hutumika kupunguza maumivu makali ya mifupa.
 
Madhara anayoweza kupata mgonjwa kutokana na aina hii ya tiba ni pamoja na kushindwa kusimamisha uume au uhanithi, kukosa hamu ya kula, uchovu, ngozi kubabuka, kuharisha na kutoa mkojo uliochanganyika na damu.
 
Tiba ya Homoni
Hii ni aina ya tiba inayotumia dawa zinazopunguza kiwango au ufanyakazi wa homoni ya testosterone mwilini. Testosterone ni homoni ya kiume inayochochea ukuaji wa tezi dume, hivyo basi matumizi ya dawa hizi husaidia kupunguza ukuaji huu na kusambaa kwa seli za saratani.
 
Tiba ya homoni hutolewa kwa wanaume walio katika hatua za mwisho za ugonjwa huu kwa nia ya kupunguza maumivu na kutibu dalili za ugonjwa. Dawa zinazotumika kwa tiba ya aina hii zimegawanyika katika makundi mawili, zile zinazochagiza uzalishaji wa homoni ya luteinizing (luteinizing hormone-releasing hormones, LH-RH) kwa mfano goserelin, nafarelin na leprolide; na zile zinazozuia ufanyaji kazi wa homoni ya androgen kwa mfano flutamide, bicalutamide na nilutamide.
 
Madhara yanayoweza kusababishwa na utumiaji wa dawa hizi ni pamoja na kichefuchefu na kutapika, upungufu wa damu, kuongezeka uzito, uhanithi na kukosa hamu ya tendo la ngono, matatizo katika ini na matiti kuwa makubwa.
 
Baadhi ya madaktari hutumia upasuaji wa kuondoa korodani kama njia ya kupunguza kiwango cha homoni za kiume mwilini kwa kigezo kwamba kiwango kikubwa cha homoni hizi huzalishwa kwenye korodani. Hata hivyo tiba hii haifanyiki mara kwa mara.
 
Baada ya matibabu?
Baada ya matibabu, mgonjwa wa saratani ya tezi dume hufuatiliwa kwa ukaribu kuhakikisha kuwa saratani haisambai sehemu nyingine za mwili. Ufuatiliaji hujumuisha mgonjwa kufanyiwa uchunguzi wa mara kwa mara pamoja na kupima PSA kwa kipindi cha miezi mitatu mitatu mpaka mwaka mmoja.