Ulega: Ulaji wa nyama na mayai ya kuku wa kisasa hauna madhara


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema kuwa ulaji wa mayai ya kuku wa kisasa hayana madhara kwa binadamu.

 Ulega alisema hayo akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalum, Zainab Mndolwa (CUF). Alisema zipo aina mbili za ufugaji ambazo ni ufugaji wa kienyeji na ufugaji wa kisasa na kuongeza kuwa ufugaji wa kuku wa kisasa hutumia dawa nyingi sana katika ukuzaji na hutumia muda wa wiki tatu hadi nne ndio huliwa na binadamu.

Katika swali lake la msingi Zainab alitaka kufahamu iwapo kuku hao wana madhara gani kwa binadamu na je, Serikali inamkakati gani wa kuwasaidia wafugaji wa kuku kutumia njia bora ya kisasa ambayo haina mashaka kwa watumiaji? Akijibu swali hilo Ulega alisema, Napenda kulijulisha Bunge lako tukufu kwamba ulaji wa nyama ya kuku au mayai ya kuku wa kisasa hauna madhara. Aidha, ufugaji wa kuku wa kisasa hauendani na matumizi ya dawa kwa wingi.

Alisema vyakula vinavyotumika kwenye kulisha kuku wa kisasa huwa ni viini lishe kama madini, vitamin, protini na nishati pamoja na chanjo ambazo sio dawa ambayo ni muhimu kwa ukuaji na afya ya kuku na havina madhara kwa afya ya mlaji.