Uuzaji wa mali za wanandoa usiozingatia sheria chanzo cha migogoro Lindi


Na. Ahmad Mmow ,Kilwa.

UUZWAJI wa mali usiozingatia sheria na kukosekana ushirikishwaji kwa wanandoa katika kufanya uamuzi wa mali zilichumwa kwa pamoja ni chanzo cha migogoro katika jamii mkoani Lindi.

Hayo yameelezwa leo na ofisa mradi wa kupinga ukatili wa kijinsia wa shirika la msaada wa kisheria kwa wanawake na watoto Lindi (LIWOPAC), Michael Mwanga wakati wa semina ya uundwaji wa sheria ndogo zinazopinga ukatili wa kijinsia.Iliyofanyika katika mamlaka ya mji mdogo wa Kilwa Kivinje.

Mwanga amesema jamii lazimza izingatie sheria katika uuzaji wa mali za pamoja hasa zilizochumwa na wanandoa. Kwani miongoni mwa sababu zinazokwamisha kasi ya utendaji wa shuguli za maendeleo ni migogoro inayotokana na uuzwaji holela wa mali hizo.

Ameongeza kuwa licha ya kusababisha migogoro lakini pia uuzaji mali kiholela unasababisha dhuluma baina ya washirika katika utafutaji wa mali hizo kwani wengi wanaouza mali kiholela hawawashirikishi washirika wenzao waliochuma nao mali wanazouza.

Alitoa wito kwa viongozi wa vijiji na mitaa wahakikishe wananchi hawauzi mali bila kuzingatia sheria.Bali wajiridhishe kwamba wauzaji wameshirikisha washirika wao kabla ya kusaini nyaraka za mikataba za mauziano.

Mwanga alitoa wito mwingine kwa viongozi wa ngazi hiyo ya utawala mkoani humu watambue wajibu wao wakutoa na kufikisha elimu kwa jamii kuhusu ukatili wa kijinsia,uzingatiaji sheria katika uuzaji wa mali za pamoja na ushirikishaji katika kupanga matumizi ya mapato.

Nae ofisa ufuatiliaji wa mradi huo,Nelson Choaji alisema uzoefu unaonesha hakuna ushirikishaji katiika kupanga mapato na matumizi hali ambayo inasababisha migogoro.Huku akiweka wazi kwamba tabia hiyo inafanywa na watu wa jinsia zote.

"Hata wanawake wanaingia na kukopa kwenye vikoba bila kuwashirikisha waume zao.Mambo yakiwachachia zinataifishwa mali walizochuma na waume zao.Viongozi saidieni kutoa elimu,"alisema Choaji.

Kwaupande wake diwani wa kata ya Kilolambwani,Karim Nyanga alisema kwasasa mauziano ya mali katika vijiji vingi yanafanyika katika ofisi za setikali za vijiji na mitaa.Hivyo nirahisi kuwadhibiti watu wanaouza mali bila kuwashirikisha wenza wao.

 Alisema ni wajibu wa viongozi wa vijiji kujiridhisha kama ushirikishaji ulifanyika.Huku akitoa wito kwa mamlaka zinazotunga sheria kutunga sheria itayozuia mali zilizouzwa na kununuliwa bila kuwashirikisha washirika zisitambuliwe kama zimeuzwa na kununuliwa kihalali.

Maelezo yaliyoungwa mkono na mtendaji wa kijiji cha  Pande ploti,Mohamed Sheha aliyesema migogoro inayotokana na kukosekana ushirikishaji wa maamuzi katika kupanga matumizi ya mali zapamoja kunachangia kushusha ufanisi wa utendaji shuguli za kiuchumi.Huku akihaidi kutoa elimu kwa wananchi wakijiji anachoongoza kuhusu madahara ya ukatili wa kijinsia na kutokuwepo ushirikishaji wa kupanga matumizi ya mali za pamoja.

Washiriki wa semina hiyo ya siku moja walikuwa ni wenyeviti,watendaji wa vijiji vya na wawakilishi wa wasaidizi wa kisheria(mabalozi) wa vijiji vya Pande ploti,Dimba,Mikoma na Kilolambwani.Wengine ni madiwani wa kata za Pande na Kilolambawani.