Viongozi Mizigo wapewa onyo Uchaguzi Mkuu 2020

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Hamphrey Polepole amesema licha ya ushindi mkubwa wanaoendelea kuupata kwenye chaguzi mbalimbali, lakini hawatakua tayari kuwarudisha viongozi mizigo kwa wananchi katika uchaguzi mkuu mwaka 2020.

Polepole aliyasema hayo leo Jumanne Novemba 6, 2018 wakati akizungumza na wajumbe wa kamati za siasa mkoa na wilaya ya Kusini Unguja visiwani Zanzibar katika ukumbi wa mkutano wa TC Dunga.

Alisema wabunge na madiwani pamoja na wawakilishi wa CCM wanapaswa kujitathmini wakifahamu wana jukumu kubwa la kuwaletea maendeleo wananchi.

"Chama chetu hakikuwapa nafasi ya uongozo kama zawadi ili mwende mkale bata, tumewapa nafasi ya kuwatetea wananchi wenu na kutetea ilani ya chama chetu" alisema.

Pamoja na hayo, Polepole aliwataka watendaji wa Serikali wakiwamo wakurugenzi wa manispaa na viongozi wengine wa wilaya na mikoa kuhudhuria vikao vyote vya chama kueleza utekelezaji wa ilani ya chama katika majukumu yao.

Alisema haiwezekani kuona wana CCM wanafanya kazi halafu kuna watendaji wanashindwa kuwajibika ipasavyo.

Polepole alisema watendaji hao wanapofanya vibaya lawama kubwa inawenda kwenye chama ambacho ndiyo chenye kutekeleza ilani yake.