Waziri Jafo apiga marufuku mila ya wafiwa kutakaswa kwa kufanya tendo la ndoa


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI),  selemani Jafo amekemea mila ya wafiwa kutakaswa kwa kufanya tendo la ndoa na mtu mwingine ili kuondoa mkosi kwenye kisiwa cha Ukara kwa kuwa wanaweza kupata maambukizi ya Virusi vya Ukimwi(VVU) na ugonjwa wa Ini.

Waziri Jafo amekemea tabia hiyo inayoendelea kisiwani humo kwasasa baada ya watu wengi kufiwa na wenza wao kutokana na ajali ya kivuko cha MV. Nyerere kilichozama miezi michache iliyopita na kupoteza watu wengi.

Katika ziara yake maalum ya utekelezaji wa agizo la Rais Dk. John Magufuli la ujenzi wa majengo yenye hadhi ya  hospitali katika eneo la Ukara, Waziri Jafo amesema zoezi hilo limeanza rasmi leo na kuagiza  ujenzi huo ukamilike ndani ya miezi mitatu.

Amesema amepata taarifa kwamba wafiwa wanafanya mapenzi na watu wengine ili watolewe mikosi kitendo ambacho ametahadharisha kwamba kinaweza kusababisha maafa makubwa kisiwani humo kutokana na watu wao kuambukizwa nagonjwa yakiwepo gonjwa la UKIMWI na Ugonjwa wa Ini yaani Hepatitis B.

Jafo amewataka wale  ambao bado hawajafanya kitendo hicho cha kutakaswa wasijaribu kabisa kwani kinaweza kusababisha maafa makubwa kisiwani humo.