https://monetag.com/?ref_id=TTIb Zana haramu za uvuvi 28,958 zakamatwa Mwanza | Muungwana BLOG

Zana haramu za uvuvi 28,958 zakamatwa Mwanza


LICHA ya kutolewa elimu kwa wavuvi kuhusu matumizi sahihi ya zana zinazotakiwa katika uvuvi Ziwa Victoria, lakini baadhi wamekuwa wakikaidi na kuendelea kutumia dhana haramu.

Hali hiyo inathibitishwa na kukamatwa na kuteketezwa kwa zaidi ya zana haramu za uvuvi 28,958 zenye thamani ya Sh. milioni 697 katika kisiwa cha Ghana wilayani Ukerewe mkoani Mwanza.

Akizungumza wakati akiteketeza zana hizo kisiwani hapo, Ofisa Mfawidhi wa Ulinzi wa Rasilimali za Uvuvi Kanda ya Ziwa, Didas Mtambalike, alisema wameendelea kutoa elimu kuhusu zana zinazotakiwa kwenye uvuvi kwa manufaa ya taifa na kizazi kijacho.

Alisema inatakiwa zitumike nyavu kuanzia inchi 6 zenye macho 26, dagaa wavu unaohitaji ni milimita 8, huku ndoano ukubwa wa namba 9 hadi 11, lakini kumekuwapo na baadhi wanaotaka kujinufaisha wakiendelea kutumia zilizo chini ya kiwango, hali inayosababisha kuvuliwa samaki wachanga.

Alisema operesheni hiyo ilifanyika kwa mujibu wa Sheria ya Uvuvi namba 22 ya mwaka 2003 na kanuni zake za mwaka 2009 na kwamba tangu kuanza kwa operesheni Sangara Januari mwaka huu katika ziwa hilo, imesaidia hupatikanaji wa samaki na dagaa tofauti na miaka ya nyuma.

“Natumia fursa hii kuwaonya na kuwasihi kuacha kutumia zana hizo kwa kuwa operesheni ni endelevu na itasitishwa endapo tutaona uvuvi haramu umeisha kabisa ziwani,” alisema.

Naye Ofisa Mfawidhi Ulinzi wa Rasilimali za Uvuvi Kanda ya Ukerewe, Judith Mgaya, alisema katika operesheni hiyo ya siku mbili walifanikiwa kukamata zana haramu za uvuvi kutoka kwa watuhumiwa 12, zikiwamo nyavu za samaki (makira) 7,750, nyavu za dagaa 8, ndoano 21,200 na mashine 37.

“Tumepata idhini ya mahakama inayotupa ruhusa kuteketeza zana hizo baada ya wamiliki kuzitelekeza na kushindwa kujitokeza,” alisema.

Mmoja wa wavuvi kisiwani hapo, Michael Bukali, alisema wanaunga mkono serikali katika operesheni hiyo kwa sababu na wao hawapendi uvuvi haramu, isipokuwa changamoto iliyopo ni wauzaji wa zana hizo ambao wanabandika nembo ambazo hazioneshi ukuweli kuhusu vipimo vinavyotakiwa.

Aliiomba serikali kuanza kuuza zana za uvuvi kwa kuwa ina wataalamu ambao wanaweza kufanya ukaguzi viwandani zinapotengenezwa nyavu pamoja na madukani wanapoziuza.

Alisema kwa kufanya hivyo, itaiwezesha serikali kutambua tatizo lililopo ili kudhibiti uvuvi haramu katika Ziwa Victoria.