Afisa Mtendaji aswekwa Selo na Waziri Lugola kwa kutafuna fedha za Wananchi


Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amemsweka ndani Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Namalebe, Kata ya Chitengule, Jimbo la Mwibara, wilayani Bunda, kwa kosa la kutafuna fedha za wanakijiji wilayani humo.

Waziri Lugola ambaye ni Mbunge wa jimbo hilo alitoa maamuzi hayo katika mkutano wa hadhara na wananchi hao uliofanyika kijijini hapo leo, baada ya kuwataka wananchi wenye malalamiko, maswali pamoja na ushauri watoke mbele ili aweze kuwasikiliza wananchi hao.

Baada ya agizo hilo, zaidi ya wananchi kumi walijitokeza na kuuliza maswali pamoja na kutoa kero zao, ndipo watu saba kati ya waliotoka mbele wakiwa wamepanga foleni walitoa tuhuma mbalimbali kuhusiana na Afisa Mtendaji wa Kijiji hicho, Wilbard Malea kutafuna fedha zikiwemo fedha za maendeleo ya kijiji pamoja na za faini kutokana na mashtaka yanayowasilishwa na wananchi kwake kwa ajili ya usuluhishi pamoja na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Mkazi wa Kijiji hicho, Simon Joseph alimtuhumu katika mkutano huo, Mtendaji huyo alimfuata katika kikundi chao cha Muungano cha kuweka na kukopeshana alisema anaomba kukopa fedha shilingi 91,000 na kijiji kitarudisha fedha hizo, lakini mpaka leo hajazilipa na hakutumwa na Serikali ya Kijiji bali alisema uongo ili ajipatie kwa njia ya udanganyifu.

Pia Happyness Tabonwa mkazi wa kijiji hicho, alimlalamikia mtendaji huyo amechukua mbuzi wake watatu baada ya kushindwa kulipa shilingi 50,000, akaamua kuwakamata mbuzi hao na baada ya kumpeleka elfu 50 anayoidai Mtendaji huyo akashindwa kuwarudisha mbuzi hao kwa kuwa alishawauza na pesa kazitafuna.