Kauli ya Yanga kuhusu mchezo wao wa kesho

KOCHA WA YANGA, MWINYI ZAHERA.

KOCHA wa Yanga, Mwinyi Zahera, amesema ingawa atawakosa nyota wake, Kelvin Yondani na Raphael Daudi kwenye mchezo wa kesho, bado wanauwezo wa kuendeleza rekodi yao ya kutopoteza mchezo kwenye ligi.

Kesho Yanga wataumana na Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa taifa ukiwa mchezo wao wa 16 msimu huu baada ya kucheza michezo 15 bila kufungwa.

Akizungumza na gazeti hili baada ya mazoezi ya jana asubuhi, Zahera alisema kuwa atamkosa Yondani kutokana na kuwa na kadi tatu za njano na Daudi ni majeruhi.

“Hawatacheza Jumapili (kesho) lakini wapo wachezaji wengine wenye uwezo wa kucheza namba zao na kila kitu kikaenda sawa,” alisema Zahera.

Alisema lengo lao ni kuendeleza rekodi waliyoanza nayo ya kutopeteza mchezo na hilo wana uhakika wataliendeleza mbele ya mashabiki wao.

Katika hatua nyingine kiungo mpya wa timu hiyo, Haruna Moshi ‘Boban’ jana alianza mazoezi kwenye timu hiyo.

Boban, nyota wa zamani wa Simba, amejiunga na Yanga kwa mkataba wa miezi sita akitokea African Lyon.

Yanga wanaongoza ligi wakiwa na pointi 41 kutokana na michezo 15 waliyocheza wakiwazidi Azam FC kwa pointi moja.