Maandamano yasababisha mamia ya watu kujeruhiwa huku mabenki, migahawa na masoko yakifungwa kutokana na vurugu

Waziri wa mambo ya ndani wa Ufaransa Christophe Castaner amesema watu wapatao 118 pamoja na maafisa wa polisi 17 wamejeruhiwa katika maandamano yaliyofanyika jana.

Katika mkutano na waandishi wa habari waziri huyo alisema jumla ya watu 125,000 walishiriki maandamano hayo nchi nzima, watu 974 wanashikiliwa na polisi kutokana na maandamano hayo.

Ulinzi uliimarishwa nchi nzima kabla ya maandamano magari mengi yenye silaha yalishiriki doria, Jumla ya wana usalama 89,000 walishiriki kulinda doria, kati ya hao 8000 walitumika jijini Paris.

Siku ya jumamosi waandamanaji wakivalia vizibao vya rangi ya njano mpauko walikusanyika mbele ya Champs-Elysees jijini Paris. Mabenki, migahawa pamoja na masoko vilifungwa kutokana na vurugu.

Polisi walitumia mabomu ya machozi kutawanya waandamanaji waliokuwapo Champs-Elysees. Katika maandamano hayo ya Jumamosi mara kadhaa polisi na raia walishikana mashati.

Maelfu ya waandamanaji waliovalia vizibao vya njano wamekusanyika katika miji mikubwa nchini Ufaransa ikiwapo Paris tangu Novemba 17 kupinga agizo la rais Emmanuel Macron kupanisha bei ya mafuta, pamoja na kupinga hali ya mdororo wa uchumi katika taifa hilo.

Waandamanaji wengi wao ni wakazi wa maeneo ya vijijini kutokana na gharama kubwa za makazi ya mijini, wamemtaka rais Macron kuondoa kodi hiyo kwenye mafuta pamoja na kuboresha hali ya kiuchumi.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanyikahivi karibuni asilimia 84 ya wafaransa,  haswa haswa  wenye kipatocha kati wanaunga mkono maandamano hayo.

Bei ya mafuta nchini Ufaransa  imepanda kwa zaidi ya  asilimia 20 mwaka huu.