Naibu Waziri aagiza ukarabati wa barabara ya Dom-Moro kukamilika haraka


Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, amemtaka mkandarasi wa kampuni CGI Contractors Limited anayekarabati barabara ya Dodoma- Morogoro sehemu ya Magubike na Gairo kuhakikisha anakamilisha kazi hiyo mapema ili kupunguza adha ya msongamano wa magari katika eneo hilo.
Agizo hilo amelitoa leo wilayani Gairo mkoani Morogoro akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua miundombinu inayosimamiwa na sekta yake katika mikoa ya Dodoma na Morogoro ili kujionea maendeleo yake.

Aidha, Naibu Waziri Kwandikwa amemsisitiza mkandarasi huyo kuchukua tahadhari katika kipindi hiki cha mvua ikiwa ni pamoja na kuhakikisha ujenzi wa barabara hiyo unakuwa imara hususan katika sehemu za miinuko ili kuzuia ajali zinazoweza kutokea katika maeneo hayo. "Hakikisheni mnamaliza haraka ukarabati wa barabara hii, magari hapa yamekuwa mengi na msongamano ni mkubwa, mnachotakiwa kufanya kwa sasa ni kufuatilia taarifa za hali ya hewa ili muweze kukabiliana na mvua na huku mkipanga ratiba zenu kuhakikisha mnakamilisha kazi hii mapema", amesema Naibu Waziri Kwandikwa.

Akiwa njiani kuelekea mkoani Morogoro katika eneo la Kibaigwa (panda mbili) mjini Dodoma, Naibu Waziri Kwandikwa amekagua madaraja yanayojengwa na Wakala wa Barabara ( TANROADS), mkoani humo na kuwapongeza kwa ujenzi wa madaraja hayo ili kudhibiti maji yanayotuama hapo hususan katika kipindi cha mvua na kusababisha kero kwa watumiaji wa barabara hiyo. Ameongeza kuwa kwa mwaka huu wa fedha 2018/ 2019, Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu kuhusu ujenzi wa barabara ya Dodoma - Morogoro kutokana na mahitaji ya barabara hiyo kuonekana kuwa ni makubwa kutokana na ongezeko la watu na magari mara baada ya Serikali kuhamia Dodoma.