Omba omba 43 wakamatwa kufuatia operesheni ya RC Ayoub



Jumla ya watu  43 wanaosadikiwa kuwa omba omba wamekamatwa katika Mkoa wa Mjini Magharibi kati hao 13 wanatoka Tanzania Bara na wengine wanatoka katika Wilaya ya Magharibi “A”: na “B” Kisiwani Unguja.

Zoezi hilo limefanyika kufuatia kuenea kwa omba omba  wengi katika viunga vya Mkoa wa Mjini Magharibi na baadhi yao kuonekana kukaidi kuachana na biashara hio ya omba omba kufuatia maagizo mbali mbali ya yaliyotolewa hapo awali na uongozi wa Mkoa huo .

Akizungumza na watu hao katika ukumbi wa sebleni kwa wazee  Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Ayoub Mohammed amesema zoezi la kuwakusanya omba omba katika Mkoa wake limefanikiwa na kusisitiza shughuli hiyo ya omba omba haikubaliki katika maeneo hayo na endapo mtu yeyote antakaehusiaka anafanya shughuli hiyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

Amesema serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaendelea kutimiza wajibu wake kuwajengea mazingira bora wananchi wake ikiwa ni pamoja na kuimarisha ustawi wa jamii,hivyo si vyema kuona baadhi ya wananchi wanajingiza katika mambo yasiyokubalika na kupelekea kupoteza utu wao

Aidha Mkuu wa Mkoa amesema uchunguzi uliofanywa umebainisha kuwepo kwa baadhi ya watu wanaojihusisha na kuleta watu kufanya biashara hiyo kutoka maeneo mbali mbali kwa lengo la kujipatia kipato jambo ambalo ni kinyume na utaratibu wa sheria za nchi na kupelekea kuharibu mila, silka na utamaduni wa Kizanzibari.

Katika hatua nyengine Mkuu wa Mkoa amesema zoezi la kuanza kuwarejesha omba omba hao kwa jamaa zao kwa upande wa Zanzibar limeanza na kwamba hatua ya kuwakamata itaendelea ili kuona hali hiyo katika Mkoa huo inaondoka kabisa.

Mapema akizungumza katika mkutano huo Mkurugenzi Ustawi wa Jamii na Idara ya Wazee Nd. Wahida Maabadi amesema wengi wa omba omba hao wanatumia hali zao ili kufanya shughuli hiyo jambo ambalo linaitia aibu Serikali kwani imekuwa ikiandaa utaratibu na mazingira mzuri wa kusaidia watu wasio jiweza na wenye mahitaji maalum.

Nao baadhi ya omba omba hao wengi wao wakiwa wanawake wameeleza kuwa hali duni na kukosa watu wa kuwasaidia na ugumu wa maisha ndio jambo linalopelekea kuingia katika biashara hiyo,hata hivyo wameomba radhi uongozi wa serikali ya Mkoa wa Mjini Magharibi na kuahidi kutoendelea na jambo hilo.