https://monetag.com/?ref_id=TTIb SMZ yapiga marufuku uvuvi haramu maeneo ya hifadhi | Muungwana BLOG

SMZ yapiga marufuku uvuvi haramu maeneo ya hifadhi



Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema uvuvi haramu katika maeneo ya hifadhi haukubaliki kwani ndiyo chanzo cha kuharibu mazingira ya baharini ikiwemo matumbawe.

Hayo yalisemwa na Waziri wa Maliasili Mifugo na Uvuvi, Rashid Ali Juma wakati alipotembelea kisiwa cha Misali kilichopo Pemba ambacho kipo chini ya maeneo ya hifadhi yanayokabiliwa na aina zote za uvuvi haramu.

Alisema kisiwa cha Misali ni miongoni mwa visiwa vichache vyenye rasilimali kubwa ya kitaifa ikiwemo hazina ya viumbe vya baharini pamoja na sekta ya utalii. Aliwataka watendaji wanaosimamia kisiwa hicho kuhakikisha kwamba wanaimarisha ulinzi wa doria za baharini na kupambana na aina zote za uvuvi haramu unaohatarisha mazalia ya samaki.

"Kisiwa cha Misali kipo chini ya mpango wa taifa wa uhifadhi wa mazingira ya baharini ambacho ni hazina kubwa kwa viumbe wa baharini na sekta ya utalii," alisema.

Mkuu wa doria katika idara ya maendeleo ya uvuvi Zanzibar, Haji Shomari alisema doria katika kisiwa cha Misali zimeimarishwa kwa sababu kisiwa hicho kipo jirani za nchi ya Mombasa. Alisema yamejitokeza matukio ya baadhi ya watalii na wavuvi kutoka nchi jirani kuingia katika kisiwa hicho bila ya kibali huku wavuvi wengine wakifanya matukio ya uharibifu wa mazingira.

Shomari alikitaja kisiwa cha Misali kuwa miongoni mwa visiwa tegemeo ambavyo viumbe kama Kasa ni moja ya sehemu ya mazalia yao lutokana na utulivu mkubwa uliopo. “Moja ya kazi kubwa ya kikosi cha doria ni kuimarisha ulinzi katika eneo la kisiwa cha Misali ambapo tumekuwa makini sana katika kupambana na uvuvi haramu,” alisema.