Viongozi wote lazima wafuate ilani ya CCM - Juma Mabodi


Naibu Katibu  Mkuu  wa Chama cha Mapinduzi Abdullah Juma Mabodi amesema viongozi wote wanaongoza katika sehemu zao za kazi lazima wafuate ilani ya Chama Cha Mapinduzi.

Hayo aliyasema wakati akizungumza na watendaje wa baraza la Manispaa Mjini Zanzibar huko katika ukumbi wa Sebleni wakati alipokuwa akifanya ziara katika sehemu mbali mbali za Mkoa wa Mjini Magharibi kukagua miradi ya maendeleo ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi.

Alisema lengo kuu la ziara hiyo ni kutizama miradi ya maendeleo na mapato yanayokusanywa na Baraza la Manispaa Mjini katika Mkoa wa Mjini Magharibi na kutaka kujua ugatuzi unatumika vipi ikiwemo masuala ya elimu, afya pamoja na vyoo katika sehemu zilizokuwa muhimu.

Pia alitaka kujua jinsi ya pesa za mfuko wa Jimbo zinavyotumika katika miradi ya maendeleo katika sehemu mbali mbali za manispaa hiyo.

Nae Mkurugenzi wa Manispaa Mjini, Said Juma Ahmad alielezea maendeleo yaliyopatikana katika manispaa hiyo alisema kwa upande wa sekta ya afya ya mama na mtoto wameimarisha huduma hiyo kwa jumla ya vituo 4 vimefanyiwa matengenezo ili kuweka mazingira bora ya utolewaji wa huduma wa vituo hivyo .

Alisema vituo hivyo ni pamoja na Chumbuni kumefanyiwa matengenezo ya choo, Jango’mbe kumefanyiwa matengenezo ya paa na mfumo wa maji safi na salama , Sebleni uwekaji wa umeme unaotumia nguvu za jua  na Mpendae matengenezo yaliyofanywa ya chumba cha kutolea huduma za meno.

Pia alisema chanjo tofauti za mama na mtoto zimesambazwa katika vituo 10 vya Serikali , vituo viwili binafsi na vituo vitatu vya kijeshi pamoja na kutolewa chanjo ya pepo punda kwa wanafunzi wa kike ambao wamefikia umri wa kujifungua katika skuli za Faraja, Jango’mbe , Mwembeladu , Kidongochekundu na Benmbella.

Vile vile mikutano ya tathmini za shughuli za Afya na vifo vya mama na mtoto imefanyika pamoja na kufanya mikutano ya kujitathmini kwa watendaji juu ya kuhamasisha kinamama kuhudhuria klinik na chanjo za watoto.

Hivyo Mkurugenzi alisema jumla ya Tsh. 661,267 ,703 zimeingizwa kwa ajili ya kutekeleza miradi mbali mbali inayosimamiwa na Mfuko wa jimbo kwa Wilaya ya Mjini kwa mwaka 2016, 2017  na nusu ya mwaka 2018 kati ya fedha hizo Tsh. 681,922, 654 sawa na asilimia 103 zimetumika kwa miradi mbalimbali ikiwemo maji safi na salama , afya , kusaidia wajasiriamali , matengenezo ya njia za ndani na kusaidia elimu.

Naibu Katibu Mkuu  wa Chama Cha Mapinduzi Abdullah  Juma  Mabodi akiwa katika ziara yake hiyo ya siku moja  alitembelea kituo cha Afya Sebleni, kikundi cha wakulima Amani kwa Wazee, Soko la machinjio Darajani na Skuli ya Msingi ya Kidongo Chekundu.