Wizara ya Afya yasitisha uhamisho



Waziri wa Afya Zanzibar, Hamad Rashid amesema wamesitisha maombi ya uhamisho kwa watumishi wa wizara hiyo ikiwemo madaktari waliopo Pemba kwenda kufanya kazi Unguja.

Mohamed ameyasema hayo wakati akitoa ufafanuzi kuhusu kuwepo kwa tatizo la madaktari na wafanyakazi wengine wa kada ya afya Pemba kuomba uhamisho mara kwa mara.

Amesema wafanyakazi wengi wa afya wanapoajiriwa kufanya kazi Pemba hutekeleza masharti ya kazi, lakini katika kipindi cha mwaka mmoja au miwili huanza kuomba taratibu za uhamisho.

Alizitaja sababu kubwa za kuomba uhamisho kwa wafanyakazi hao ambao wengi ni wanawake ni ndoa.

Tunapata matatizo makubwa kwa watumishi wa kike ambapo wanapoajiriwa huchukua muda wa miaka miwili na kuolewa na kulazimika kuomba uhamisho kwa madai kuwa wanaume zao wapo Unguja," amesema.

Alifahamisha kwamba Wizara ya Afya tayari imepata kibali cha kuajiri jumla ya wafanyakazi 762 wa kada tofauti ambapo kisiwa cha Pemba kimepewa kipaumbele kujaza nafasi mbalimbali.

Amesema matarajio makubwa ya wizara kwamba tatizo la uhaba wa watumishi wa kada mbalimbali katika sekta ya afya Pemba litapungua kutokana na kuwepo kwa ajira hizo.

Tumepewa nafasi za kuajiri wafanyakazi 762 katika kada mbalimbali ambapo wapo watakaoajiriwa Pemba ili kukabiliana na uhaba wa wafanyakazi hasa madaktari," amesema.

Amesema tatizo la uhaba wa madaktari katika kisiwa cha Pemba lipo zaidi katika hospitali za vijijini ikiwemo Micheweni ambapo wafanyakazi wa afya wanapoajiriwa katika kipindi kifupi huanza kuomba uhamisho kwa visingizio mbalimbali.