ZFA imelazimika kusimamisha baadhi ya michezo kutokana na kuharisha ghafla kwa wachezaji!



Na. Thabit Madai, Zanzibar.

Ligi kuu soka Zanzibar imelazimika kusimamisha baadhi ya michezo kutokana na kuzuka kwa maradhi ya tumbo na kuharisha kwa wachezaji timu ya Mwenge (Pemba) na Mbuyuni(Pemba).

Akizungumza na Mwandishi wetu kwa njia ya Simu Mwenyekiti wa Kamati ya ligi  ZFA Hussein Ali Ahmada amekiri kutokokea kwa maradhi hayo kwa wachezaji wa timu hizo mbili zinazoshiriki ligi kuu soka Zanzibar ambazo ni Mwenge kutoka Pemba na Timu ya Mbuyuni ya Pemba.

Alisema mara ya kupokea kwa Taarifa hizo iliwalazimu kufunga safari na kwenda kuangalia hali ilivyo katika kambi walizofikia mara baada ya kuingia katika kisiwa cha unguja na kukuta kuwa wachezaji wa timu hizo wanasumbuliwa na maradhi hayo.

“tulipofika kikwajuni walipofikia timu ya Mbuyuni tuliwakuta kuwa wameshahama mara baada ya wachezaji kuumwa kwa matumbo na kuharisha kwa upande wa mwenge pia hali ilikuwa hivyo hivyo wanaumwa na kuharisha takribani nusu ya kikosi chao” alisema Mwenyekiti wa Kamati ya mashindano.

Aidha alisema  wamejaribu kufuatilia ripoti ya daktari imesema kuwa chanzo cha maradhi hayo mpaka sasa hakijajulikana kama chakula, vinywaji au vyoo walivyokuwa wanatumia wakati wa safari ya kuja unguja kwa michezo yao ya ligi kuu soka Zanzibar.

“uvumi unaendelea si sahihi kwani Daktari ameshindwa kuthibitisha vyanzo vya maradhi hayo kwa timu hizo zote mbli” alisema.

Kwa upande wake Katibu wa kamati ya Mashindano ya ZFA taifa Alawi Haidari Fumu alielezea hali ya ugumu wa fedha kwa vilabu vinavyoshiriki ligi kuu soka Zanzibar na kusema kuwa hali haipo vizuri hata kidogo na hii inasababishwa na ligi kuendeshwa bila ya ufadhili wowote.

“hamna asiejua kama timu zetu zipo katika hali ngumu ya kifedha na hii inasabaishwa kuwa ligi kuu Zanzibar haina mdhamini ligi inajiendesha wenyewe” alisema Alawi.

Aidha Alawi alieleza kuwa wakati walipokuwa wanakagua timu hizo moja ya hali walikutana nayo ni kuwa wachezaji iliwabidi wapelekwe hospitali wachache na wengine watumie dawa walizoandikiwa wenzao kutokana na kuwa vilabu havina pesa.

Jitihada za kuwatufuta viongozi wa timu hizo iligonga mwamba kutokana kuwa hawakuwa wakipokea simu.