Aliyeshika nafasi ya pili apinga matokeo ya Urais Congo


Martin Fayulu, mgombea urais wa upinzani DRC aliyeibuka wa pili, ameyakataa matokeo yaliyotangazwa na tume ya taifa ya uchaguzi.

Matokeo ya awali yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (CENI) yanaonesha Felix Tshisekedi alipata asilimia 38.57 ya kura zilizopigwa.

Bw Tshisekedi alipata zaidi ya kura 7 milioni naye Bw Fayulu akapata kura takriban 6.4 milioni, huku mgombea wa serikali Emmanuel Ramazani Shadary akimaliza wa tatu akiwa na takriban kura 4.4 milioni.

Bw Fayulu ameambia Idhaa ya Kifaransa ya BBC kuwa: "Hii ni kashfa mbaya sana. Matokeo haya hayana uhusiano hata kidogo na ukweli halisi. Raia wa Congo hawataukubali utapeli kama huu daima. Felix Tshisekedi hakupata kura 7 milioni, haiwezekani. Alizitoa wapi?"