DR Congo yakataa kuchelewesha matokeo ya uchaguzi

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imekataa katakata wito uliotolewa na Muungano wa Afrika AU kucheleweshwa kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa urais.

Muungano wa Ulaya AU unasema kuwa una wasiwasi mkubwa kuhusu uadilifu wa matokeo ya mapema ambayo yalimpatia ushindi Felix Tshisekedi.

Kiongozoi mwengine wa upinzani Martin Fayulu ameitaka mahakama ya kikatiba kufutilia mbali matokeo hayo akidai kwamba ndiye mshindi wa uchaguzi huo.

Ni wazi kwamba wito wa AU wa kufutilia mbali matokeo hayo umeikasirisha serikali.

Msemaji wa serikali Lambert Mende amesema kuwa mahakama ya kikatiba ilikuwa huru na hakuna mtu mwenye haki ya kuielekeza.

Muungano wa Ulaya unasema kuwa mwenyekiti wake , rais wa Rwanda Paul Kagame na viongozi wengine wataelekea Kinshasa kutafuta suluhu ya mgogoro huo.

Bwana Mende alisema kuwa ujumbe huo unakaribishwa lakini akasisitiza kuwa matokeo hayo ya baada ya uchaguzi hayatabadilishwa.

Hiyo inamaanisha kwamba kuapishwa kwa Felix Tshisekedi kutafanyika katika kipindi cha siku chache zijazo iwapo mahakama ya kikatiba itaunga mkono ushindi wake.

Muungano wa Afrika (AU) awali ulikuwa umeitaka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kuahirisha kutangaza matokeo ya uchaguzi mkuu.

Muungano huo unaonuia kuhimiza umoja na demokrasia, unasema una "shaka kubwa" na matokeo ya awali yaliotangazwa wiki iliyopita.

Matokeo hayo yalimpa ushindi mgombea wa upinzani Felix Tshisekedi lakini mpinzani wa utawala uliopo, Martin Fayulu, anasisitiza kuwa yeye ndiye aliyeshinda.

Matokeo ya mwisho yanatarajiwa kutangazwa leo Ijumaa.

Kumezushwa maswali mengi kuhusu uhakika wa matokeo hayo huku kukiwepo shutuma kwamba Tshisekedi anapanga mpango wa kugawana madaraka na rais anayeondoka Joseph Kabila.

Baadhi ya viongozi katika Muungano wa Afrika na serikali walikutana katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa jana Alhamisi na kutoa tamko kuhusu uchaguzi huo wa Desemba 30 unaopingwa pakubwa.

"Kumekuwa na shaka kubwa kuhusu namna matokeo ya awali yalivyokusanywa, kama ilivyotangazwa na tume huru ya kitaifa ya uchaguzi kwa kura zilizopigwa," taarifa ya muungano huo imesema.

"Kadhalika, AU imetaka kuahirishwa kutangazwa kwa matokeo ya mwisho ya uchaguzi mkuu huo," iliongeza taarifa.

Fayulu anatuhumu kwamba mshindi wa muda bwana Tshisekedi alikubaliana na rais anayeondoka Joseph Kabila.

Kabila amehudumu kwa miaka 18 na matokeo, iwapo yatathibitishwa, yataidhinisha ukabidhi wa kwanza wa uongozi kwa mpangilio tangu taifa hilo lipate uhuru kutoka kwa Ubelgiji mnamo 1960.

Tume ya uchaguzi imesema Tshisekedi alishinda 38.5% ya kura, ikilinganishwa na 34.7% alizoshinda Fayulu. Mgombea wa muungano wa serikali Emmanuel Shadary alijizolea 23.8%.

Matokeo hayo yanatarajiwa kutangazwa kama ni mapema sana leo, na wataalamu wanasema kuna uwezekano wa matokeo matatu.

Huenda mahakama:

Ikathibitisha ushindi wa Tshisekedi
Ikaagiza kura kuhesabiwa upya
Ikafutilia mbali matokeo yote na kuitisha uchaguzi mpya