Fahamu faida 10 za kuoga maji ya baridi


Watu wengi hupenda kuogea maji ya moto, hii ni kutokana na kuogopa baridi au sababu za kimazoea tu. Ingawa mara nyingi umekuwa ukisisitiziwa kuwa maji moto yana manufaa mengi, lakini hata maji ya baridi nayo yana manufaa yake.

Je uko tayari kuongeza maarifa au hata kubadili mtazamo wako? Karibu nikushirikishe faida 10 za kuogea maji ya baridi.

1. Huongeza utayari
Maji ya baridi hukufanya uchangamke, hili ni tofauti na maji ya moto. Mara nyingi mtu anapoogea maji ya baridi hasa baada ya kuamka humfanya awe katika hali nzuri ya kuwa tayari kuendelea na majukumu yake.

Kumbuka hata wakati wa kuoga maji baridi kasi ya upumuaji hubadilika na kukufanya kuongeza kiasi cha oksijeni kinachoingia mwilini.

2. Hulainisha ngozi na nywele
Maji moto huchubua ngozi na nywele, hasa kwa kuondoa mafuta laini yanayolinda ngozi na nywele na kuvifanya viwe vikavu sana.

Kwa kuoga maji ya baridi, ngozi na nywele zako havitapaushwa bali vitasafiwa na kuachwa katika hali nzuri ya kupendeza.

3. Huboresha kinga mwili
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Thrombosis Research Institute, ulibainisha kuwa watu wanaoogea maji ya baridi wanaongeza uzalishaji wa seli nyeupe za damu.

Utafiti huu unaeleza kuwa kutokana na kuongezeka kwa kiwango cha metaboli mwili unapojaribu kujipasha moto, ndipo seli hizi nyeupe ambazo hupambana na maradhi zinapozalishwa.

4. Huhamasisha kupunguza uzito
Kupunguza uzito? Ndiyo kupunguza uzito. Baada ya binadamu kula vyakula, kiasi fulani huhifadhiwa mwilini kama mafuta. Baadhi ya mafuta haya huyeyushwa na kutumiwa kuupasha mwili joto.

Hivyo kuoga maji ya baridi kutawezesha aina fulani ya mafuta kuyeyushwa ili kuzalisha joto mwilini, jambo ambalo litapelekea kupungua kwa uzito.

5. Huchangia katika afya ya misuli
Wanamichezo wanafahamu kuwa kuoga maji baridi baada ya michezo au mazoezi huwafanya wajisikie vizuri mapema. Hili ni kutokana na maji baridi kuhamasisha mzunguko wa damu ambao huiwezesha misuli kujijenga tena upya vyema.

6. Huondoa msongo wa mawazo
Utafiti uliofanyika kwenye chuo cha tiba Virginia, ulibaini kuwa kuogea maji baridi huzalisha kemikali ya noradrenaline ambayo husaidia kukabili msongo wa mawazo.

7. Hulinda afya ya uzazi ya wanaume
Utafiti uliofanyika umebainisha kuwa wanaume wanaoogea maji ya moto kwa muda wa nusu saa hupungukiwa mbegu za kiume kwa kiasi kikubwa baada ya kipindi cha miezi sita. Hili ni kutokana na mbegu za kiume kuwa rahisi sana kuathiriwa na joto.

Utafiti huo unaongeza kuwa wanaume walioacha kuogea maji ya moto kati ya hao waliochunguzwa, kiasi cha mbegu za kiume kiliongezeka kwa asilimia 491. Je bado huoni manufaa ya maji ya baridi? Naamini sasa umeshaaza kuyaona.

8. Hukusaidia kulala vyema
Je umeshawahi kuogea maji baridi ukiwa umechoka sana au umefanya kazi ngumu? Kama umeshawahi kuogea maji baridi ni wazi kuwa ulijisikia vizuri na ukalala vizuri pia.

Hili ni tofauti na maji ya moto kwani badala ya kukupooza na kukufanya ulale vyema yatakufanya uchemke na kuchoka zaidi.

9. Huboresha mzunguko wa damu
Mtu anapokuwa anaoga kwa maji baridi mapigo ya moyo huenda kasi na kusababisha damu kuzunguka vyema kwenye maeneo mbalimbali ya mwili.

Mzunguko mzuri wa damu utaondoa vile visivyotakiwa na kuleta vile vinavyotakiwa kwenye viungo na sehemu mbalimbali za mwili wako.

10. Hurudisha nguvu za mwili
Mara nyingi mtu anapokuwa amechoka, kwanza huhitaji kuoga ili ajisikie vizuri. Ni wazi kuwa mtu anapooga hasa kwa maji baridi hujisikia kurudiwa na nguvu au hali nzuri kuliko ile aliyokuwa nayo kabla ya kuoga.

Ikiwa umechoka na unatokwa na jasho, hebu jaribu kuogea maji baridi nawe utashuhudia swala hili.

Naamini umepata maarifa juu ya faida za kuogea maji baridi. Naamini sasa hakuna haja ya kuongeza foleni za maji jikoni wakati unaweza kuogea maji ya baridi na ukapata manufaa yaliyoelezwa hapa.

Kumbuka!

Ikiwa una tatizo la msingi la kiafya kama vile maradhi yatokanayo na baridi au tatizo lingine la kiafya linaloathiriwa na baridi, ni vyema ukaogea maji ya moto au ya uvuguvugu.