Lady Jaydee azungumzia kifo cha Oliver Mtukudzi


Msanii wa muziki wa Bongo Fleva, Lady Jaydee amesema Oliver Mtukudzi alikuwa msanii mrahisi
kufanya naye kazi kutokana na tabia yake ya kumpokea mtu jinsi alivyo.

Oliver Mtukudzi msanii nguli Afrika kutokea nchini Zimbabwe alifariki dunia hapo jana akiwa ametoa albamu zaidi ya 50 kwenye maisha yake ya kimuziki.

Akizungumza na Idhaa ya Kiswahili ya BBC, Lady Jaydee amesema mara baada ya kukutana na Oliver Mtukudzi alimshauri vitu vingi kuhusu muziki kitu ambacho kimempa faida.

"Baada ya hapo mambo yalibadilika kutokana na ushauri aliyonipa, namna ya kufanya muziki wa live na kuhusisha vinjo vya Kiafrika kwenye muziki wangu," amesema Lady Jaydee.

"Ni mtu wa kawaida ambaye si mgumu kufanya naye kazi, kila binadamu ana mambo yake lakini ni mtu mrahisi sana kufanya naye kazi, anampokea kila mtu anavyokuja," ameeleza.

Je, Walikutania wapi? 

Lady Jaydee ameeleza kuwa kwa mara ya kwanza alikutana na Oliver Mtukudzi nchini Afrika Kusini katika utoaji wa tuzo za Kora.

Mwaka 2010 Lady Jaydee alimshirikisha Oliver Mtukudzi katika wimbo wake uitwao Mimi ni Mimi. Producer wa wimbo huo, Man Walter kutoka studio za Combination Sound amemshukuru Lady Jaydee kwa kumpatia nafasi ya kufanya kazi na nguli huyo wa muziki Afrika.

"Asante sana Lady Jaydee kwa kuniamini kuifanya kazi yako 2010 - 2011, Mimi ni mimi (I am Who I am) uliyomshirikisha Legendary huyu,dah hakika iliniongezea kujiamini kwenye Live Sound mpaka sasa,"  ameandika  Man Walter kwenye ukurasa wake wa Instagram.