Taasisi na madhehebu ya dini yafutiwa kodi ya pango la Ardhi


Serikali imefuta kodi ya pango la ardhi kwa Taasisi na Madhehebu ya dini nchini kuanzia mwaka wa fedha wa 2018/2019.

Taarifa hiyo imetangazwa jana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe.William Lukuvi Jijini Mbeya wakati wa ibada ya kuwaweka wakfu viongozi wa Jumuiya Kuu ya Kanisa la Kibaptisti Tanzania (BCT).

Waziri Lukuvi amesema Rais Magufuli ameiagiza wizara hiyo kutoyatoza kodi madhehebu ya dini kwa sehemu ambazo zimeandaliwa kwa ajili ya kufanyia ibada.

"Rais ameagiza kuanzia Julai mosi mwaka huu wa fedha madhehebu ya dini yasilipe kodi ya ardhi kwa maeneo ambayo huduma za maombi na ibada zinatolewa, hata hivyo msamaha huu hauhusu maeneo ambayo kuna miradi ya kuingiza fedha ambayo tunajua madhehebu mengi yameanzisha," amesema Lukuvi.

Lukuvi amefafanua maagizo hayo tayari yametolewa kwa makamishna wa ardhi wa kanda na mikoa pamoja na maofisa ardhi wa majiji, manispaa na halmashauri nchi nzima.Hata hivyo, Lukuvi ametoa nafasi ya kukutana na viongozi wa dini ambao wana migogoro ya ardhi kwenye maeneo ambayo wanatoa huduma.