.

1/18/2019

Tumeibiwa mno, hakuna siri tumechapwa kweli - Rais Magufuli


Rais John Magufuli amesema alitengua uteuzi wa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dkt. Ally Simba kutokana na kutosimamia kwa ukamilifu utekelezwa wa Mfumo wa Kusimamia Uwazi katika Mawasiliano ya Simu.

Rais Magufuli amesema hayo leo wakati wa hafla ya makabidhiano ya Mfumo mpya wa kusimamia uwazi katika mawasiliano ya simu.

Mfumo huo unaosimamiwa na Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) utahakiki mapato yote ya watoa huduma za mawasiliano na kugundua mawasiliano ya simu ya ulaghai.

"Mwanzoni wakati naingia madarakani sikuridhishwa sana na utendaji wa TCRA, palikuwa na mchezo mbaya sana, tumeibiwa mno, hakuna siri tumechapwa kweli, tumeliwa kweli," amesema Rais Magufuli

Katika hatua nyingine Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Eng. James Kilaba ambaye muda wake ulikuwa unakaribia kumalizika ameongezewa mkataba wa miaka mitano na Rais Magufuli.