Uzalishaji samaki waongezeka Kilwa, wavuna Kg. 234,642 kwa mwaka


Na.Ahmad Mmow, Lindi.

Uzalishaji samaki wilayani Kilwa, Lindi umeongezeka kutokana na kazi kubwa inayofanywa na vikundi shiriki vya ulinzi na usimamizi wa rasilimali za bahari na Pwani (BMU) na serikali.

Hayo yameelezwa na mkuu wa wilaya ya Kilwa, Christopher Ngubiagai alipokuwa anazungumza kwenye kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa iliyopo katika manispaa ya Lindi.

Ngubiagai alisema uwepo wa BMU umechangia kuongezeka kwa samaki katika bahari ya Hindi hasa katika maeneo ya Somanga, Songosongo, Kivinje na Masoko.

"Mazao ya uvuvi yameongezeka kutokana na jitihada kubwa zinazofanywa na vikundi hivyo kwa kushirikiana na serikali ya wilaya. Mwaka 2018 uzalishaji ulifikia kilo 234,642, kutoka kilo 65,234 za mwaka 2005,"alisema Ngubiagai.

Ngubiagai aliweka wazi kwamba ongezeko hilo la mazao ya uvuvi katika wilaya hiyo umeongeza pia mchango wa pato la ndani la halmashauri ya wilaya ya Kilwa. Kwani hadi mwaka jana (2018) sekta ya uvuvi ilichangia pato la halmashauri  Tsh. Milioni 25.00 kutoka Tsh. Milioni 11.00 ya mwaka 2005.

Mwaka jana shirika la kimataifa la usimamizi na uhifadhi wa mazingira duniani(WWF) katika kukabiliana na uchafuzi wa mazingira katika bahari ya Hindi lilikabidhi boti za kisasa kwa halmashauri za wilaya za Kilwa na Mafia ambazo zinatumika kufanya doria ambapo BMU zimepewa kipaumbele katika matumizi ya boti hizo.