.

1/12/2019

Waziri Ummy atoa onyo kwa Madaktari 'Muache kuwa madalali wa maduka ya dawa'


Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto,  Ummy Mwalimu amewaonya madaktari nchini kuacha tabia za kuwa madalali wa maduka ya dawa kwa kuwaandikia wagonjwa
dawa mara mbili mbili huku akiwaambia kwamba watakaobainika watachukuliwa hatua kali.Huku akiagiza hospitali za Rufaa kote nchini kuhakikisha zinakuwa na maduka ya dawa litakalokuwa  na uhakika wa dawa zote muhimu ili kuondosha kero hiyo na kuondoa mianya ya madaktari kudalalia dawa kwenye maduka binafsi.

Ummy ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Mkoani wa Tanga aliyasema hayo wakati akizungumza na watumishi wa Hospitali ya Mkoa wa Tanga Bombo na kauli hiyo inatokana na kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa wananchi ambao walimsimamisha nje ya hospitali hiyo kabla ya kukutana nao.

Wananchi hao ambao walikuwa wakisubiri kuingia hospitalini hapa walimueleza kero hiyo ambapo alisema mbali na kero hiyo aliwaagiza madaktari nchi nzima kuhakikisha wanazingatia mwongozo wa kutoa dawa au matibabu ili kuepusha lawama kwa wagonjwa wa kubadilishiwa dawa na kila daktari.

Akiwa kwenye eneo hilo ambalo ni maalumu kwa ajili ya kupumzikia wananchi ambao wanakwenda kuwatazama wagonjwa wao kabla ya kuingia hospitalini hapo ndipo wananchi hao walipoamua kumueleza kilio hicho ambacho kimekuwa kikiwaumiza muda mrefu sana na kumuomba akishughulikie.

“Kwa kweli hii sio sawa kabla ya hapa nimepata wasaa wa kuzungumza na wananchi nje ya geti lakini kilio chao kikubwa ni kutokuridishwa na huduma tunazozitoa likiwemo suala la mgonjwa kuandikiwa dawa na kila daktari hii sio sawa naaagiza madaktari acheni kuwa madalali wa maduka ya dawa na sitaki kusikia hili siku nyengine “Alisema Waziri Ummy.