Wizara ya Afya Zanzibar kupima afya wafanyakazi wao


Wizara ya Afya Zanzibar kwa kushirikiana na Kitengo cha Maradhi yasiyoambukiza wamefanya zoezi la kupima afya za Wafanyakazi wa Wizara hiyo lilioendeshwa na madaktari wa kichina pamoja  madaktari wazalendo wanaofanyakazi Hospitali kuu ya Mnazimmoja.
Akitoa nasaha wakati wa kuanzisha zoezi hilo, Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Harusi Said Suleiman alisema lengo la kufanya uchunguzi wa afya za wafanyakazi wa Wizara hiyo ni kuwawezesha kujua afya zao na ni moja ya njia ya kuhamasisha jamii kuona umuhimu wa kupima afya zao mara kwa mara kila inavyowezekana.
Alisema Wizara kwa kushirikiana na Kitengo cha maradhi yasiyoambukiza inampango wa kutoa huduma za aina hiyo katika taasisi nyengine kwa malengo ya kuhamasisha uchunguzi wa afya mapema kabla ya kusubiri kuugua.
Aliongeza kuwa Wizara imeamua kutoa huduma hiyo kwa wafanyakazi wake baada ya kugundulika kuongezeka kwa kasi maradhi yasiyoambukiza Zanzibar na duniani kwa jumla.
Alisema kati ya wafanyakazi 1,940 waliopimwa afya zao mwaka 2016 asilimia 6.0 waligunduliwa wakiwa na kisukari na Shinikizo la damu imefikia asilimia 33 kiwango ambacho ni kikubwa kwa mujibu wa idadi ya wananchi wa Zanzibar.
Aliwataka wafanyakazi wa Afya kujitokeza kwa wingi kupima afya zao kila fursa inapotokea kwani mfanyakazi akiwa na afya bora utendaji wake wa kazi wa kutoa huduma kwa wananchi utaimarika.
Kiongozi wa madaktari wa China wanaofanyakazi Hospitali ya Mnazimmoja Dk. Zhang Zhen alisema wataendelea kushirikiana na Wizara ya Afya kuhakikisha wanatoa huduma bora zaidi kwa wananchi wa Zanzibar.
Alisema ushirikiano kati ya China na Zanzibar ulianza miaka mingi iliyopita na lengo la nchi zote mbili ni kuona ushirikiano huo unaendelea kuimarika zaidi.
Vipimo vilivyofanyika katika zoezi hilo ni shinikizo la damu, kisukari, matatizo ya macho, masikio, kinywa pamoja na ushauri kwa magonjwa  ya akinamama na maradhi mengine sugu. Wafanyakazi waliogundulika na matatizo watapatiwa matibabu katika Hospitali kuu ya Mnazimmoja.