CHADEMA watoa tamko zito kuhusu kushikiliwa kwa Mbunge Sugu


Leo Februari 21, 2019, saa moja asubuhi, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama ambaye pia ni Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi 'Sugu', aliitikia wito wa Jeshi la Polisi, aliopewa jana kupitia kwa Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC) wa Mbeya na Mkuu wa Upelelezi Makosa ya Jinai (RCO), wote kwa nyakati tofauti, wakimtaka kufika Kituo Kikuu cha Polisi mkoani humo kwa ajili ya mahojiano.

Hadi jioni hii, tunapolazimika kutoa taarifa Jeshi la Polisi mkoani Mbeya limeendelea kumshikilia chini ya ulinzi Mbunge huyo na baada ya kwenda naye eneo la Ikuti jijini humo, ambapo inadaiwa alitoa maneno ya uchochezi siku ya Jumamosi, Februari 16, mwaka huu alipokuwa akijibu malalamiko ya kero mbalimbali za wananchi wa jimboni kwake, polisi wamemrejesha Mbunge Mbilinyi Kituo Kikuu cha Polisi na amenyimwa dhamana bila kuwepo kwa taarifa yoyote ya kunyimwa haki yake hiyo ya msingi kwa mujibu wa sheria za nchi.

Chadema kinalaanii vikali kitendo cha Mbunge kushikiliwa, kuhojiwa na sasa kunyimwa dhamana kwa kuwaahidi wananchi wake kuwa atakwenda kuhoji bungeni suala la Wamachinga kuuziwa vitambulisho, ambao ni wajibu wake akiwa mwakilishi wa wananchi.

Chama kinafuatilia jambo hili kwa ukaribu kupitia kwa wanasheria wa wake, kikilitaka Jeshi la Polisi mkoani Mbeya kumfikisha Mbunge huyo mahakamani haraka iwezekanavyo kwa mujibu wa taratibu za nchi ili apate haki yake ya dhamana.

Kwa taarifa tulizonazo, mahojiano aliyofanyiwa yalijikita kutaka kujua tafsiri ya maneno aliyoyatumia Mbunge huyo siku hiyo ya Februari 16, ambapo akisikiliza malalamiko ya wapiga kura wake, baada ya kutoa msaada wa saruji, nondo na mabati, katika Shule ya Ikuti, aliwaahidi wananchi kuwa atakwenda kuhoji bungeni suala la vitambulisho wanavyouziwa 'Wamachinga' kwa bei ya shilingi 20,000/= ili kujua msingi wake na kwanini limeanza kufanyiwa kazi bila kuwashirikisha wadau ili kuwa na uelewa wa pamoja.

Mbunge Mbilinyi alitoa majibu hayo baada ya wananchi hao, hususani wafanyabiashara ndogondogo wanaojihusisha na uuzaji wa mboga kumlalamikia usumbufu wanaoupata kwa  kulazimishwa na mamlala za kiserikali mkoani humo kununua vitambulisho vya wafanyabiashara ndogondogo kwa bei hiyo wasiyoweza kumudu kutokana na udogo wa mitaji, biashara yao na hata mapato wanayopata. Walihoji mantiki iliyotumika kuwapangia wauza mboga wanunue vitambulisho hivyo kwa bei hiyo moja, sawasawa na wafanyabiashara ndogondogo wengine wenye mitaji mikubwa kwa kuwalinganisha na wauza mbogamboga.

Imetolewa leo Alhamis, Februari 21, 2019 na;

Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA