DC Njombe: Hatuwezi kufikia uchumi wa Viwanda kama matukio haya yataendelea


Matukio ya utekaji na mauji ya watoto Wilayani Njombe  yamesababisha uchumi kuzorota kwa kushuka kwa uzalishaji mali kwa wananchi.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Ruth Msafiri jana akifunga maombi katika  Kanisa la TAG Milinze yaliyolenga kuombea Wilaya hiyo kuondokana na matukio ya utekaji na mauaji ya watoto na kusema kuwa hali hiyo inatokea kwa kuwa wazazi wanatumia muda mwingi kwapeleka watoto na kuwafuata watoto shule hivyo kupoteza muda na kusimamisha shuguli zao.

“ Hatuwezi kufikia uchumi wa Viwanda kama matukio haya yataendelea wazazi wanapoteza sana muda katika kuhakikisha watoto wao wanapata ulinzi kwa kuwapeleka na kuwarudisha nyumbani, niwaambie tu Halmashauri ya Mji wa Njombe inaoongoza katika Halmashauri zote nchini kwa kuwa na kipato kikubwa kwa mwaka mwananchi wa hapa ana uwezo wa kuwa na shillingi million 5” alisema Msafiri

Mkuu wa Wilaya huyo amewataka waumini wa Kanisa hilo na wananchi wa Wilaya na Mkoa wa Njombe kwa ujumla kuombea mkoa wao ili kuondokana na vitendo hivyo vinavyopelekea kuzorotesha shughuli za kiuchumi.

Akitoa salama za Wizara Mwenyekiti wa Timu ya Wataalam kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Idara za Maendeleo na Ustawi wa Jamii) Bi. Hanifa Selengu amesema Serikali ipo pamoja na wananchi wa Mkoa wa Njombe katika kulaani matukio hayo ya utekeaji na mauaji ya watoto yaliyojitokeza.