Dkt Angeline Mabula aipiga tafu timu ya mpira wa miguu ya Wanawake


Na James Timber.

Mbunge wa Jimbo la Ilemela ambae pia ni Naibu Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe Dkt. Angeline Mabula ameendelea kuiunga mkono Timu ya mpira wa miguu ya wasichana kutoka Jijini Mwanza inayojulikana kama Marsh Academy kwa kusaidia mafuta ya usafiri na chakula kwa wachezaji wa Timu hiyo ikiwa ni jitihada zake za kuhakikisha anaibua vipaji vya michezo mbalimbali na kuendeleza vilivyopo kwa kuandaa mazingira rafiki na wezeshi.

Akizungumza na wachezaji hao, Dkt Angeline Mabula mbali na kuwapongeza amewaasa kuongeza juhudi ili kuhakikisha Timu hiyo inazidi kuwa bora na kinara wa mafanikio katika mashindano ya ndani na nje ya nchi huku akiwahakikishia kuendelea kuwaunga mkono katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili

"Mimi kwa kushirikiana na wadau wengine tutaendelea kuwaunga mkono kama lilivyo lengo langu la kuifanya sekta ya michezo kuwa ajira rasmi kwa kuibua vipaji vipya na kuendeleza vile vilivyopo, Lakini nanyi mnao wajibu wa kuhakikisha mnapambana kushinda mashindano mbalimbali yatakayoiletea nchi sifa ndani na nje" Alisema Mabula


Aidha Dkt Mabula amewaasa wadau wengine wa sekta ya michezo kuitazama Timu hiyo kwa jicho la pekee kwa kuhakikisha wanashiriki kutatua changamoto zinazoikabili ili izidi kufanya vizuri.

Kwa upande wake mwakilishi wa Wachezaji wa Timu hiyo, Amemshukuru mbunge huyo kwa ushirikiano anaoutoa kwa Timu yao huku akimtaka kuendelea kuwaunga mkono sanjari na kuahidi mafanikio katika mashindano mbalimbali watakayoshiriki.

Wakati huo huo Dkt Angeline Mabula ameshiriki mazoezi ya viungo vya mwili yanayoshirikisha viongozi wa Serikali na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yaliyoandaliwa na Capital City Run chini ya uratibu wa Comrade Nsolo Mlozi Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Dodoma ili kupambana na maradhi mbalimbali yasiyo ya kuambukiza.